Habari za Punde

BAHARI YAVAMIA MASHAMBA YA WAKULIMA PEMBA

JUMLA ya wakulima 58 wa mpunga katika mabonde ya wapape na mangwena, Mkoa wa Kaskazini Pemba, huenda wakakosa kulima kikimo hicho katika msimu huu kutokana na mashamba yao kuingia maji ya chumvi na kujaa mchanga.

Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansoor Yussuf Himid, alielezwa hayo alipotembelea mabonde hayo kuangalia hali halisi ya kilimo hicho, sambamba na kusikiliza matatizo ya wakulima.

Akiwa katika bonde la Wapape, wilaya ya Micheweni, Waziri Mansoor, alielezwa na wakulima hao kuwa jumla ya wakulima 43 hawana pahala pakulima kwa msimu huu baada ya mashamba yao kuingia maji ya chumvi.

Mwenyekiti wa bonde hilo, Hamad Malik, alieleza kwamba pamoja na jitihada walizozichukuwa za kujenga tuta kuyazuia maji ya chumvi juhudi hizo hazikuzaa matunda.

“Mheshimiwa mabadiliko ya hali ya hewa yametuathiri sana katika bonde hili kwani pamoja na tuta unaloliona bado maji ya chumvi yamekuja kwa kasi na yanaingia katika mashamba yetu”, alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema bonde ambalo lina ukubwa wa ekari 100, zaidi ya ekari 20 tayari zimeingia maji ya chumvi hali iliyopelekea mashamba hayo kutotumika tena kwa kilimo cha mpunga katika msimu huu.

Bonde la wapape lina jumla ya wakulima 200 ambapo wanawake ni 80 na wanaume 120 na linahitaji tuta lenye urefu wa mita 230 ili kuyazuia maji ya chumvi kuingia katika mashamba ya wakulima.

Nae Waziri wa Kilimo na Maliasili, aliwaagiza maofisa wa Kilimo Kisiwani Pemba kushirikiana na wakulima wa bonde hilo ili kuhakikisha wanajenga tuta haraka iwezekanavyo ili kuzuwia athari zaidi.

Katika hatuwa nyengine katika bonde la umwagiliaji maji la mangwena liliopo nje kidogo ya mji wa Wete, wakulima wa bonde hilo walimueleza Waziri wa Kilimo na Maliasili kwamba jumla ya wakulima 15 hawana mashamba ya kulima kutokana na mashamba yao kupitiwa na ujenzi wa barabara mpya itokayo Wete –Gando.

Bwana Shamba wa eneo hilo alisema kuwa wajenzi wa barabara hawakufuata barabara ya zamani badala yake walijaza dongo katika baadhi ya mashamba ya wakulima na kupelekea wakulima kukosa pahala pa kulima.

Bonde la umwagiliaji maji la Mngwena, wilaya ya Wete lenye ukubwa wa hekta 10, linajumla ya wakulima 97 ambapo wanawake 56 na wanaume 41.

Akijibu baadhi ya hoja za wakulima wa bonde la Mangwena, Ofisa Mdhamni wa Wizara ya Kilimo Maliasili Pemba, Dk. Suleiman Shehe Mohammed, alisema tayari kumeundwa kamati ambayo itaweza kutatua tatizo hilo.

Mapema akizungumza na wakulima katika mabonde tafauti ya mpunga Kisiwani Pemba , Waziri , Mansoor Yussuf, alisema kuwa serikali itajitahidi kutatua matatizo ya wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa chakula.

“Hivi sasa lazima tuimarishe kilimo na wakulima wetu, kwani nijambo la lazima kwa vile mahitaji ya chakula yameongezeka duniani”, alisema.

Waziri huyo alisema katika kufikia azma hiyo serikali msimu ujao wa kilimo inakusudia kufikisha huduma zote muhimu kwa wakulima ikiwemo matrekta, na dawa sambamba na kuimarisha mabonde ya umwagiliaji maji

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.