Na Ashura M. Hamad (Ummu Ahmad)
Wapendwa wadau karibuni tena katika hekaya za bibi. Leo bibi anasema ubaya mbaya. Tafakari!
Hodi! Hodi! Hodi!, Mlango ulibishwa.
“Aaah hao washaanza tena hodi hodi ndio kwanza nina kaa, nyanyuka nyanyuka miguu yenyewe mibovu, mpaka wataniangusha”. Bibi alilalamika hiyo nyanyuka nyanyuka na yeye mtu mzima miguu inamuuma. Alitoka huko si muda mrefu, lakini atafanyaje ndio anachanjaruka na kila biashara ili apate mahitajio yake sio kutegemea tu na omba omba maisha haya kuchakarika.
Bibi alifanya kila aina ya biashara, hakuwa na mume, ni mjane, analea wana na mjukuu juu, il-hali apate japo pesa mbili tatu, asisubiri mwisho wa mwenzi kutabaruku anacholetewa na watoto wake wanapojaaliwa.
Bibi aliuza vifuu, kuni na makumbi, unajua zamani hakukuwa na kuka wala stima. Watu walitegemea sana kuni, vifuu, makumbi na wachache walitumia makaa. Pia alikuwa na biashara ya hina ya majani iliyotwangwa. Akipika udi wa makapi na wanja wa hapsi sana wakitumia mabiharusi. Zamani hakukuwa na piko wala tancho, warembo walitumia wanja unaopikwa kwa hapsi. Ukitaka kuijua hapsi waulize wazee wa zamani hawa waleo hawa waache tu na mapiko yao.
Biashara ya malai, barafu na maji baridi. Kwa hiyo nyumba kila wakati ilikuwa na pirika za hodi. Na hizo ndizo biashara za kusaidia maisha. Utasikia sasa watu wanalalama na maisha hupita kuomba wasaidiwe lakini hawataki kujikurupusha wavivu, kazi zao za kuchagua wakati hao wazee wetu wa zamani hawakuchagua kazi na maisha yaliwaendelea na hawakuwa wategemezi kumsubiri mtu.”Wahenga walisema mtumai cha nduguye hufa masikini” Vipi wao waliweza nasi tushindwe itabidi tujiulize.
Hodi hiyo iliyobishwa haikuwa ya biashara, alikuwa mgeni wa bibi alikuja kumtembelea akitokea sokoni kwa Haji tumbo. Alikaribishwa hadi jikoni akae kwenye kiti kwani bibi alikuwa na kazi lukuki akiziacha ataharibu kila kitu na muda haumsubiri mtu.
Niliporudi chuoni, nilimkuta mgeni wa bibi, nilimsabahi na niliwapisha na maongezi yao, mara niliitwa kukuna nazi, ikabidi nijumuike na mazungumzo yao lakini nilikuwa msikilizaji tu wa mikasa. Zilisimuliwa hadithi nyingi, visa, mikasa, waliokufa, walioolewa, walioumwa ila nilisikitishwa na kisa cha “Ubaya Mbaya.”
Hee Jamani dunia hatuonani kwa mambo kila kukicha utasikia hili na lile, dunia imebadilika, hatupendani jamani tunatendeana ubaya tu. Bibi alimlalamikia mgeni wake. Akamhadithia.
Nilikuwa safarini Pemba kwa matatizo yangu ya kilimwengu, maana watoto watatutoa roho! Kuna waliopata wana na wengine hupata watoto wakatutotoa. Tumbo huzaa mengi kama la kasa, hutoa mijusi, maguruguru, kenge kila mmoja na tabia zake, Mie nipo namsikiliza huku nakuna nazi yangu , sijui kweli ndio anavyozaa kasa au maneno ya wazee. Hapo nilipofikia kulitokea mkasa wallahi mtihani, si hadithi ni kweli.
Kulikuwa na mabibi majirani wenyewe wanasaidiana kwa hili na lile, unajua maisha ya vijijini wanashikana bado wanaishi maisha ya asili. Kumbe yule mmoja si ana chuki na mwenziwe. Sijui wamekosana nini jamani, duniani kuna siri humu. Alimdhamiria mwenziwe kumuangamiza hasa. Alilitafuta pweza lilokamilika mikia nane, akalipika akalikoleza nazi shata shata, halafu akalitia ubaya.
Alipomaliza, azma yake akaliweka vizuri na kumpelekea jirani yake. Alipofika hakumkuta. Akarudi akamfunika na kumtenga pembeni jikoni. Akenda zake kondeni.
Huku nyuma si akatokezea mtoto wake, tena ndo huyo huyo mboni ya jicho. kaolewa mjini. Kufika mamake hayupo. Akasafisha nyumba mtoto, akenda kisimani akamfulia nguo mamake, akamjazia maji. Mwana huyo kaja kwa mamake, akamfanyia kila kitu.
Alipomaliza katika kupekura pekura jikoni akamkuta pweza. Mate yakamtoka akamchukua akatia kwenye kibakuli akamla huku akijiramba, huku akimsifu mamake kwa mapishi.
Akakaa kumsubiri mamake arudi. Aliporudi mama akaona ana mgeni si haba kamsaidia kazi kwa siku hiyo alikuwa kachoka. Mtoto hakuwa na makazi tena, muda ulikwenda akamuaga mamake kabla hajaondoka akamwambia mamake, ‘Hee! Mama kumbe unajua kupika nimemkuta pweza huko jikoni kakolea’.
Mama kusikia hivyo alishtuka Paa! ‘Umekula mwanangu Hee!’ Mtoto akamwambia ‘He mama wee! nimekula kidogo nimeonja tu , nimekuletea vitoweo chungu hapo samaki usikasirike’. Mama asijue la kujibu, kapwaya wote, mwili ulimuacha. Mtoto akaondoka, huku mama kihoro kimempaa, huyo alomkusudia kumpelekea kamsahau.
Akakaa mnyonge, ilipofika usiku akaletewa taarifa mwanawe anaumwa yu taabani , hajulikani maradhi gani kavimba, tumbo si wa mkono wala mguu yupo tu mahututi. Mama alijua sababu ya mwanawe kuumwa. Masikini mtoto hakupona alifariki na mama mtu naye kihoro kilimuuwa. Jamani Ubaya mbaya umemrudia mwenyewe.
No comments:
Post a Comment