Habari za Punde

JIHAD: 'MATEJA' WASTAAFU WASHIKENI MIKONO WENZENU

Na Salum Vuai, Maelezo

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, amewataka vijana walioacha kutumia dawa za kulevya kuwa mabalozi wazuri wa kuwasaidia wenzao ambao bado wanateseka na mihadarati.

Ushauri huo aliuotoa juzi katika hafla ya kupongeza muasisi wa nyumba za kuwatibu vijana wanaotumia dawa hizo Suleiman Mauly ambaye ametimiza miaka mitano tangu azipe kisogo dawa hizo hatari.

Katika hafla hiyo iliyofanyika afisi kuu ya kampuni ya Explore Zanzibar Mbweni, Jihad alisema kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na ndio kundi linaloathirika sana kwa dawa hizo, iko haja ya kuendeleza jitihada za kuwafikia na kuwasaidia ili wabadilike na kuwa watumishi wazuri wa taifa.

Alieleza kuwa vijana waliokuwa wakitumia na baadae kuacha dawa hizo, ndio wanaoweza kueleweka vyema iwapo watakuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wenzao, kuliko watu ambao hawakuwahi kujihusisha na matumizi ya mihadarati.

"Ukitaka kumsaidia mtu mwenye matatizo mpelekee mtu anayefanana naye, nanyi mmepitia huko bila shaka mtakuwa mabalozi na walimu wazuri kwao", alisema Jihad.

Aliipongeza kampuni ya Explore Zanzibar chini ya Mkurugenzi wake Maryam Olsen, kwa kazi kubwa na ngumu wanayoifanya kuwasaidia vijana hao na kuwaandalia mustakbali mzuri wa maisha ya baadae.

Mapema Mratibu mzoefu wa harakati za mapambano dhidi ya UKIMWI na dawa za kulevya Fatma Sukwa, alieleza kufarijika kwake na mafanikio yaliyopatikana kwenye vita hivyo, akisema hayo ni matunda ya kazi alianza kujishughulisha nayo tangu mwaka 1992 katika kuwasaidia vijana wanaoathirika.

"Vijana hawa mnaowaona wameacha dawa za kulevya ni matunda ya kazi ngumu tuliyoifanya, namshukuru Suleiman kwa kuwa mhamasishaji mkubwa kwa wenziwe baada ya yeye kufahamu athari za uteja", alifafanua Sukwa.

Naye Rukia Mirza alisema Suleiman Mauly ametoka mbali na katika maisha yake yamekuwa katika kipindi kigumu, na kwamba sasa amezaliwa upya baada ya uzao wa asili pamoja na wakati alipotumbukia kwenye dimbwi la dawa za kulevya.

Akielezea namna alivyokabiliwa na hali ngumu wakati wa uteja, Mauly alisema haikuwa rahisi kwake kuachana na dawa hizo na anawashukuru wote waliomsaidia kwa njia moja au nyengine kuondokana na tatizo hilo.

Alitoa ahadi kwamba kazi aliyoanzisha itaendelea ili kuhakikisha vijana wanaotumia dawa za kulevya wanaacha na pia kuwapa elimu wasiotumia ili wasije kuangukia kwenye shimo hilo.

Mauly, aliyekuwa akitumia dawa za kulevya kwa miaka mingi, alifanikiwa kuachana nazo baada ya kupata matibabu mjini Mombasa Kenya na baadae kuhamasika kuanzisha vituo vya kubadilisha tabia kwa wengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.