Habari za Punde

MAADHIMISHO YA MIAKA 47 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Siku ya Jumatatu tarehe 26/04/2011, Tanzania itaadhimisha miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa tarehe 26/04/1964 kwa yaliyokuwa Mataifa mawili, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuungana na kuzaliwa Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya sherehe hizo Mwaka huu ambazo kitaifa zitafanyika kwenye Uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar.

Mbali na Rais Kikwete, Viongozi mbalimbali wa Kitaifa,Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wananchi kutoka Mikoa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika Maadhimisho hayo.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Marehemu Mwalimu Julius KambarageNyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 Zanzibar.

Siku ya Jumatatu tarehe 26 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.

Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwaapisha rasmi Mawaziri wapya wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27/04/1964 na tarehe 28/04/1964.

Walioapishwa tarehe 27/04/1964 ni:-

1.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Abeid Amani Karume kuwa Makamu wa kwanza wa Rais,Rashid Mfaume Kawawa, Makamu wa Pili wa Rais. Wengine na Wizara zao kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Paul Bomani(Fedha),Solomon Nkya Eliufoo(Elimu),Michael Mawbray Kamaliza(Kazi), Job Malecela Lusinde(Mambo ya Ndani), Abdulrahman Mohammed Babu(Ofisi ya Rais), Idrissa Abdulwakil(Habari na Utalii),Aboud Jumbe Mwinyi(Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais).

Wengine ni Hassan Nassor Moyo(Sheria), Abdallah Kassim Hanga(Viwanda). Mawaziri walioapishwa Tarehe 28/04/1964 ni; Derrel Noel Brycson(Afya), Amir Habib Jamal(Ofisi ya Rais),Asanterabi Nsilo Swai(Ofisi ya Rais),Oscar Salathiel Kambona(Mambo ya Nje), Jeremiah Sam Kasambala(Biashara), Said Ali Maswanya(Kilimo),Lawi Nangwanda Sijaona(Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais), Austin Kapere Shaba(Serikali za Mitaa) na Isaac Bhoke Munanka(Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Tarehe 29/04/1964 Rais Nyerere kwa wakati huo alimuapisha Kaluta Amri Abeid kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mila. Tarehe 5/05/1964 alimwapisha George Clement Kahama kuwa Waziri wa Mawasiliano, tarehe 14/05/1964 Rais Nyerere alimwapisha Tewa Said Tewa kuwa Waziri wa Ardhi na tarehe 01/06/1964 Rais alimwapisha Hasnu Makame kuwa Waziri wa nchi katika Wizara ya Mambo ya nchi za nje.

Tarehe 28/10/1964 Jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

Tarehe 29/10/1964,Rais wa Tanzania kwa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza rasmi jina la ‘TANZANIA’

Wananchi wa Tanzania walipiga kura katika Uchaguzi wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1965.

IMETOLEWA NA:

IDARA YA HABARI(MAELEZO)

ZANZIBAR, TANZANIA

22/04/2011

1 comment:

  1. Haya mie yangu n macho tu kwani hii ina nembo ya serikali.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.