Habari za Punde

MADIWANI WADAI KULIPWA POSHO 'KIDUCHU'

Na Masanja Mabula, Pemba

UMOJA wa Madiwani Zanzibar umeitaka serikali ya Mapinduzi kuliangalia suala la maslahi yao kuifanyia marekebisho sheria namba 4 ya mwaka 1995 ya halmashauri za wilaya na mabaraza ya miji ili iweze kwenda sambamba na kazi wanazofanya.

Wakizungumza kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Chake-Chake na kuwajumuisha Wenyeviti na Makamo wa Halmashauri za wilaya na Mabaraza ya miji, walisema kuwa posho wanalolipwa madiwani ya shilingi 30,000 kila baada ya miezi 3 halikidhi haja kutokana na ugumu wa kazi wanazofanya.

Walisema iko haja kwa serikali kuwalipa posho kila baada ya mwezi Madiwani kwani kazi wanazofanya za ukusanyaji wa mapato ni ngumu na zinachukua muda mwingi katika utekelezaji wake.

“Iko haja kwa serikali kuliangalia suala la maslahi ya Madiwani kwani wanafanya kazi ngumu ya kukusanya mapato ya halmashauri na mabaraza ya miji , na posho la shilingi 30,000 kila baada ya miezi 3 halikidhi haja kabisa’’, alisema Diwani Machano Fadhil Machano.

Akizungumzia sheria namba 4 ya mwaka 1995, Diwani huyo alisema sheria hiyo imepitwa na wakati na kwamba inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iiende na wakati uliopo.

Alisema wakati umefika kwa serikali kujali maslahi ya madiwani pamoja na kuwajengea mustabali mwema wa maisha yao baada ya kumaliza muda wao wa uongozi katika wadi zao.

Katika kikao hicho Wenyeviti hao walifanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi watauongoza umoja huo kwa kipindi cha miaka 5 ijayo ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chake-Chake, Omar Bakar Omar alichaguliwa kuwa Mwenyekiti naye Masuod Abrahman Masuod akachaguliwa kuwa msaidizi Mwenyekiti .

Nafasi ya katibu alichaguliwa Machano Fadhil Machano (Babla) naye Abdalla Ali Said amechaguliwa kuwa msaidizi katibu huku Amina Ali Mohamed amechaguliwa kuwa mshika fedha akisadiwa na Fatma Mohamed.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.