Habari za Punde

MOTO ULIOWASHWA CCM HAUTAZIMIKA - MUKAMA

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amesema moto uliowashwa ndani ya chama hicho siyo nguvu ya soda na hautazimika hadi imani dhidi ya chama iweze kurejea kwa Watanzania wote.

Katibu huyo alitoa Kauli hiyo jana hapo Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la wazee wa CCM Zanzibar ikiwa ni mfululizo wa utambulisho wa wajumbe wapya wa sekretarieti ya kamati kuu ya NEC.

Alisema moto uliowashwa na CCM hivi karibuni umelenga katika kurejesha tena imani kwa wananchi na hatimaye kukiona kuwa chama hicho ndio chama pekee ambacho kitakuwa kimbilio la wanyonge badala ya kuwa cha matajiri.

Alisema ili kufikia azma hiyo, CCM imejipanga vizuri na kupitia sekretarieti hiyo ya Kamati Kuu ya NEC, iliyosheheni wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali, chama kitabuni mbinu na mikakati madhubuti itakayosaidia kurejesha haiba yake iliyopotea miongoni mwa wananchi.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar, Mzee Machano Ame, aliiisifu hatua ya kujivua gamba kulikofikiwa na viongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho.

Mzee huyo aliwataka Viongozi wa CCM wa ngazi ya Mikoa hadi Tawi nao wawe tayari kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.