Habari za Punde

MTANGAZAJI MKONGWE JOSEPH ASAMA AFARIKI ZANZIBAR

MTANGAZAJI Mkongwe wa Zanzibar Joseph Caitan Asama (79) amefariki dunia jana mchana nyumbani kwake Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Marehemu Asama alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu na alizidiwa jana mchana wakati akiwa katika matayarisho ya kwenda Hospitali ya Mnazi mmoja kwa matibabu na hatimae kufariki.

Misa ya marehemu Joseph itafanyika kesho mchana katika kanisa la Angilkana Mbweni na kutarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi Unguja saa 9:00 za alaasiri.

Viongozi mbali mbali wa juu wa Serikali pamoja na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria katika mazishi ya mtangazaji huyo mkongwe wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (S.T.Z).

Marehemu Asama alianza kazi katika miaka ya mwishoni mwa 50 katika Idara ya Habari na Utangazaji akiwa katika sehemu ya utangazaji ya Sauti ya Unguja kabla ya kuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar.

Ukiacha uzoefu katika utangazaji, marehemu Joseph alikuwa Mkuu wa vipindi wa STZ, mwandishi wa habari wa Rais wa Zanzibar na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Utangazaji pamoja na Afisa Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.

Marehemu ameacha kizuka na watoto wawili, mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu Joseph Caitan Asama.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO

3 comments:

  1. Imekuwaje huyu mtangazaji mkongwe ikawa baadhi yetu wenye umri wa miaka 40 tukawa hatumjui. Mimi sijawahi kumsikia akitangaza Radio Zanzibar.Alitangaza SYZ miaka ipi na laikuwa akitangaza kipindi gani?

    ReplyDelete
  2. Labda wadau wenye kumbukumbu watusaidie ambao bado wanamkumbuka Mzee Joseph alipokuwa akinguruma Sauti ya Tanzania Zanzibar

    Hapa tunawakusudia wakongwe vile vile

    ReplyDelete
  3. M/MUNGU AILAZE ROHO YA JOSEPH ASAMA MAHALA PEMA PEPONI AMINA.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.