Habari za Punde

WAAFRIKA TUMIENI SOKO LA NDANI - DK SHEIN

· Auambia Mkutano wa Wawekezaji Afrika

· Mazingira Z’bar yaruhusu uwekezaji

Na Rajab Mkasaba, Dar es Salaam

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapnduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa nchi za Afrika kulitumia soko la ndani la fedha badala ya kutegemea zaidi soko la nje ambalo limeonekana kukabiliwa na changamoto nyingi hivi sasa.

Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati akifunga mkutano wa tisa wa Uwekezaji wa nchi za Afrika katika ukumbi wa ‘Mlimani City’ jijini Dar-es-Salaam.Katika hotuba yake, hiyo ya ufungaji Dk. Shein alisema kuwa uzoefu umeonesha kwamba soko la nje la fedha limekuwa na changamoto nyingi ambazo zimetokana na msukosuko wa kiuchumi.

Alisema kwa kawaida misukosuko ya kiuchumi inayozikumba nchi zinazoendelea pia, imekuwa ikileta athari za moja kwa moja kwa nchi hizo. Dk. Shein alisema kutokana na hali hiyo nchi za Afrika zina haja ya kuimarisha zaidi soko lake la ndani.“Ni lazima tujifunze kutokana na uzoefu tuliopata uliotokana na msukosuko wa kifedha wa dunia ambao uliathiri sana fedha za uwekezaji za nje katika eneo letu”, alisema Dk. Shein.

 Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Afrika imepiga hatua kubwa katika kuweka mazingira mazuri yaliyoiwezesha sekta binafsi kukua ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu, kuipa uwezo rasilimali watu ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mabaraza yake ya biashara, katika mikakati yao ya kuimarisha uchumi yamekuwa yakisisitiza uungwaji mkono wa sekta binafsi pamoja na kuimarisha ubia.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa maazimio yaliyotolewa katika mkutano huo ni muhimu na yataongeza ushirikiano na nguvu katika utekelezaji na uimarishaji wa uwekezaji kwa nchi za Afrika. Dk. Shein amewataka washiriki wa mkutano huo kuzitumia vizuri fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya eneo la Afrika Mashariki kwa kuamini kwamba faida inayopatikana kutokana na uwekezaji vitega uchumi ni kubwa.

Pia, Dk. Shein amewataka washiriki wa mkutano huo kuwa na mawasiliano baina yao na Mamlaka ya Vitega Uchumi na Jumuiya za wafanyabiasahara wenye viwanda na wakulima ili waweze kufahamu fursa za uwekezaji ambazo zinajitokeza mara kwa mara katika eneo hilo.Dk. Shein alishauri kufanya ziara za mara kwa mara kwa lengo la kujifunza na kubadilishana mawazo kwa ajili ya mustakabali mzima wa kuimarisha biashara na uwekezaji katika nchi za Afrika.

Akizungumza kuhusu Zanzibar, Dk. amesema kuwa kuwepo kwa amani na utulivu Zanzibar ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya uwekezaji katika sekta mbali mbali za maendeleo.Akitoa maelezo yake mafupi katika mkutano huo ambao Mwenyekiti wa mkutano huo ni Rais wa Burundi, Piere Nkurunziza, Dk. Shein alisema kuwepo kwa amani na utulivu Zanzibar ni hatua moja wapo ya kivutio kikubwa cha uwekezaji.
 
Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha sekta ya uwekezaji inapata mafanikio makubwa kwa kuiwekea mazingira mazuri. Alisema miongoni mwa mazingira hayo ni pamoja na kuweka Wizara husika inayoshughulikia sekta nzima ya uwekezaji pamoja na kuwepo kwa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
 
 Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar vipaumbele vyote vya sekta ya maendeleo vinahitajika ikiwa ni pamoja na elimu, afya, miundombinu, maji, kilimo na vyenginevyo.Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa mbali na hatua hizo zilizochukuliwa pia, suala zima la Utawala Bora nalo limeweza kuchukua nafasi nzuri kwa upande wa Zanzibar hatua ambayo imeweza kuchangia kuwepo kwa mazingira bora ya uwekezaji.
 
 Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa hatua za makusudi pia, zinachukuliwa katika kuhakikisha wawekezaji wa ndani nao wanapewa kipaumbeleza zaidi ili waweze kuwekeza nchini mwao.Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa vile Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza kupata mafanikio makubwa sambamba na mashirikiao ya pamoja ya taasisi za uwekezaji katika suala zima la kuiimarisha sekta hiyo.
 
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza alisema kuwa Jumuiya hiyo imepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja a kuendeleza ushirikino na uhusiano mwema kati ya wanachama wake sanjari na kujijengea mustakabali mzuri kiuchumi.
 
Kwa upande wa Zanzibar akitoa maelezo juu ya mkutano huo, Mkurugenzi wa ZIPA, Salum Nassor alisema kuwa Zanzibar ina maeneo mengi ya uwekezaji hasa katika sekta ya utalii, uvuvi na kilimo hasa cha mboga mboga kutokana na uhaba wa ardhi yake.
 
Alisema Zanzibar ni visiwa vilivyozungukwa na bahari hivyo uwekezaji katika sekta ya uvuvi nayo inaweza kuchukuwa nafasi kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo kwa kiwango kkuwa cha samaki katika mzunguko wa visiwa hivyo
 
.Alisema kuwa juhudi pia, zinachukulwia katika kuhakikisha zao la karafuu nalo linapewa kipaumbele katika kuhakikisha nalo linawekwa katika jumla ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kutokana na umuhimu wake mkubwa.
 
Sambamba na hayo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa serikali tayari imeweka maeneo ya vitega uchumi kwa upande wa Unguja na Pemba ambayo yako katika hali nzuri na mazingira bora kwa uwekezaji.
 
Katika mkutano huo wa siku mbili viongozi mbali mbali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walihudhuria akiwemo Rais wa Burundi ambaye ndiye Mwenyekiti wa EAC kwa sasa Rais Pierre Nkurunzinza, Rais wa Kenya, Mwai Kibaki, Rais wa Uganda,Yoweri Museven, Waziri Mkuu wa Rwanda Bernad Makuza na viongozi wengineo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.