Na Rajab Mkasaba
CHINA imeahidi kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza azma yake ya kuekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kimaendeleo. Balozi mdogo mpya wa China, Chen Yiman aliyasema hayo jana wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Balozi Yiman alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa kuongeza idadi ya madaktari ambao watawahusisha madaktari waliopata mafunzo ya lugha ya kiswahili ili iwe rahisi kuwasiliana na jamii wakati wanapotoa huduma za afya.
Aidha, alisema kuwa nchi yake itasaidia kuanzisha Idara ya majeruhi na matibabu ya dharura katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja na Hospitali ya Abdala Mzee iliyopo Pemba. Balozi Yiman alisema kuwa China imefurahishwa na uhusiano uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza katika kuzidisha uhusiano huo nchi hiyo inatarajia kuleta jopo la wawekezaji kwa madhumuni ya kuzungumza na Mamlaka ya Vitega Uchumi na Maeneo Huru Zanzibar (ZIPA) juu ya maeneo ya uwekezaji na masharti yake.
Alieleza kuwa miongoni mwa shughuli kubwa watakazofanya wawekezaji hao wakati watakaofika Zanzibar ni pamoja na kuangalia bidhaa za viwanda kwani nchi hiyo imeshaonesha utayari wa kununua mazao ya viungo yanayopatikana Zanzibar.
Kwa vile China tayari imeshapiga hatua katika sekta ya Utalii pia, nchi hiyo imekubali kuwahamasisha watalii na wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuitembelea na kuekeza katika sekta hiyo hapa Zanzibar. Kwa upande wa sekta ya elimu alisisitiza azma ya kuongeza nafasi za masomo pamoja na kujenga skuli nyengine ya kisasa kama ile iliyojengwa kwa msaada wa nchi hiyo huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Balozi huyo alisisitiza kuwa nchi yake itasaidia kuwajengea uwezo wataalamu wazalendo kwenda kujifunza nchini humo pamoja na kuahidi kuendelea kutoa misaada kwa Zanzibar ikiwemo kusaidia miradi ya usambazaji maji vijijini. Nae Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara yake ya Afya ina lengo la kuanzisha kitengo cha kushughulikia maradhi ya figo, moyo na saratani hivyo ahadi hiyo ya China ya kuiunga mkono sekta hiyo kutasaidia kufikia lengo lililokusudiwa.
Alisema kuwa kwa upande wa hospitali ya MnaziMmoja serikali inaendelea na mikakati ya lengo lake la kuifanya hospitali hiyo kuwa ya hospitali ya rufaa na ile ya Abdalla Mzee kuwa hospitali ya Mkoa Dk. Shein alisema kuwa hatua ya China kuleta ujumbe wa wawekezaji na wafanyabiashara itasaidia kuimarisha sekta hizo za maendeleo ambapo kwa kupitia (ZIPA), wawekezaji hao watapata kujua kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya uwekezaji hapa Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii hivyo ni fursa nzuri kwa watalii wa China kuja kuitembelea Zanzibar. Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia balozi huyo kuwa Serikali itampa mashirikiano ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kueleza kuwa inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na China ambao aliahidi kuendelezwa.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, jana alimuapisha Ibrahim Mzee Ibrahim kuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, hafla iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika hafla hiyo viongozi kadhaa walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud.Kabla ya uteuzi huo, Ibrahim Mzee alikuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi ambaye aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007, baada ya kustaafu kwa Katibu wa Baraza hilo, Khamis Juma Chande.
No comments:
Post a Comment