Habari za Punde

KIBWENI KUKOMESHA MADANGURO

Na Ramadhan Himid, POLISI


WANANCHI wa Kibweni wilaya ya Magharibi wamesema wako tayari kuimarisha kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu ikiwemo ukahaba ambao umekuwa kero kubwa katika Shehia yao.


Waliyasema hayo wakati wakizungumza na Kamishna wa Polisi, Mussa Ali Mussa katika kikao cha kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii ngazi ya Shehia chenye lengo la kupunguza uhalifu katika maeneo yao.


Wananchi hao walikiri kwamba kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii pindi zikitumiwa vizuri zina mchango mkubwa katika kupunguza kero mbali mbali za uhalifu.


Fatma Suleiman Bakari alimueleza Kamishna wa Polisi kuwa katika shehia ya Kibweni uhalifu kwa ujumla umepungua ila kuna tatizo la madanguro ya ukahaba ambayo yanahitaji nguvu za pamoja ili kukomesha vitendo hivyo viovu.


“Tatizo kubwa ninaloliona mimi katika shehia yetu ya Kibweni ni kwamba uhalifu umepungua lakini tuna tatizo la madanguro ambayo ni hatari kwa vizazi vyetu’’, alisema.


Naye Mohammed Abdalla Khamis, alimhakikishia Kamishna wa Polisi kuwa wataimarisha kamati za ulinzi na usalama ili kuondosha kero mbali mbali ikiwemo dawa za kulevya na kumtaka kuimarisha ulinzi maeneo ya bandarini na viwanja vya ndege ili kuzuia uingiaji wa dawa hizo.


Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema iwapo kamati hizo zitafanya vikao mara kwa mara, kupeana taarifa na kuzipatia ufumbuzi taarifa hizo, vitendo vya kihalifu vinaweza kutoweka lakini kama wataendelea kuoneana muhali miongoni mwao watajikuta wakiishi katika hali ya wasi wasi.


Alisema kamati za ulinzi, usalama na ustawi wa jamii ndio mwarobaini wa kutatua kero mbali mbali katika maeneo yao, hivyo jambo muhimu kwa wananchi wa Kibweni ni kujipanga na kuacha muhali dhidi ya wale wanaofanya vitendo hivyo.


Aidha aliwataka wananchi hao kuunga mkono falsafa ya Polisi Jamii kwani majeshi yote duniani yenye sura ya upolisi yamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa kuwashirikisha wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.