Habari za Punde

TUNAJIPANGA KUBADILI HISTORIA AFRIKA - MAFUNZO

Na Donisya Thomas
SIKU chache baada ya klabu ya soka ya Mafunzo kutwaa ubingwa wa Zanzibar, uongozi wa timu hiyo umesema kazi iliyoko mbele yao sasa, ni kuhakikisha wanafuta aibu ya kufanya vibaya kwa timu za Zanzibar kwenye mashindano ya kimataifa.

Ofisa Michezo wa jeshi hilo Makame Faki Fadau, ameliambia gazeti hili ofisini kwake Kilimani, kwamba anafahamu ugumu wa kazi hiyo lakini ana imani kuwa hakuna lisilowezekana na ni jukumu lao kuipeperusha vizuri bendera ya Zanzibar.

Fadau alifahamisha kuwa licha ya awali kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Zanzibar baada ya kuchapwa na Miembeni mabao 2-1, lakini wanamshukuru Mungu kutokana na matokeo ya mwisho ya ligi hiyo yaliyowapa taji la mwaka 2011/12.

Kuhusiana na mwenendo mzima wa ligi ndogo ya Zanzibar, Ofisa huyo alisema, ligi ya mwaka huu haikuwa na mvuto kutokana na kukosekana kwa wafadhili, pamoja na kuchezwa kwa mkondo mmoja.

Aidha alieleza kutofurahishwa na mpango wa Chama cha Soka Zanzibar kuteremsha daraja timu nyingi kwa vile hazikuwa na mechi nyingi za kushindana na hivyo kusema ingekuwa vyema timu mbili au moja tu ndiyo ingelishuka badala ya tatu.

Kwa upande wa waamuzi, Fadau alisema hawakuwa makini, na kwamba walichangia kuvuruga baadhi ya michezo kwa makusudi wakionesha dhahiri kuzibeba na kuzikandamiza baadhi ya timu.

Aliishauri ZFA kufanya kazi ya ziada kuhakikisha ligi kuu msimu ujao inapata wafadhili ili kuzipunguzia mzigo klabu zinazoshiriki kwa kuwa bila udhamini hakuna faida inayopatikana na timu zinashiriki katika mazingira magumu.

Baada ya kuukwaa ubingwa wa soka Jumatatu iliyopita, Mafunzo inatarajiwa kuiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati 'Kagame' mwaka ujao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.