Habari za Punde

UNYANYASAJI WAONGEZA WATOTO WA MITAANI

Na Mwantanga Ame

MKE  wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Seif Iddi, amesema kukuwa kwa tatizo la watoto wa mitaani kumechangiwa na vitendo vya unyanyasaji vya baadhi ya walezi kukataa kuwapa malezi mazuri watoto na kusababisha kukimbia majumbani mwao.

Mama Asha aliyasema hayo kijiji cha watoto yatima  cha S.O.S Mombasa Wilaya ya Magharibi Unguja, katika sherehe ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi wa kijiji hicho waliotumikia kwa muda mrefu ambapo kijiji hicho kimefikia miaka 20 tangu kuanzishwa kwake Zanzibar.

Alisema hatua waliyochukua wafanyakazi wa kituo hicho kwa kuwatumika watoto hao kwa muda mrefu ni jambo zuri kwani hivi sasa kumekuwa na watoto wengi wa mitaani waliokimbia majumbani mwao baada ya walezi wao kuwanyanyasa.

Alisema hivi sasa watoto wengi wanakimbia majumbani mwao baada ya kuzidiwa na manyanyaso na kuona kuishi maisha ya mitaani ni bora zaidi kuliko majumbani mwao.

Alisema hii inatokana na utamaduni wa walezi kuacha kuwapenda watoto hasa inapotokea watoto hao wazazi wao wanapofariki kwa wanaoachiwa jukumu la kuwapa malezi mazuri huwageukia na kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji.

Alisema wengi wa watoto wanaonekana kuranda mitaani baadhi yao sio kama hawana familia zao, lakini wamezikimbia kutokana na unyanyasaji wanaoupata vikiwemo vitendo vya adhabu za kikatili.

Alisema hali nyengine inayosikitisha kuwafanya watoto kukimbia majumbani mwao ni kutokana na baadhi ya walezi hao kuwachukulia mali za wazazi wao na kuwafanya kukosa msingi wa maisha yao hasa sehemu za kukaa.

Kuwepo kwa vitendo hivyo Mama Asha alisema ni mambo ya kusikitisha kuona jamii hivi sasa imekuwa ikijali mali zaidi na kuwaacha watoto wakiwa wanateseka mabarabarani wakipita kuomba.

Mama Asha alisema  ili kutokomeza  matatizo hayo ni vyema jamii ikajirudi kuona suala la malezi linakuwa ni la wote kwani haitapendeza kuona Zanzibar inakuwa na watoto wa aina hiyo kunakosababishwa na walezi.

Alisema hatua ya Mama wa Kijiji hicho kujitolea kuifanya kazi hiyo ya ulezi wanapaswa kupongezwa kwa kukubali mazingira ya aina zote za kuishi nawatoto vyema kwa kuhakikisha wanapata malezi bora.

Alisema suala la malezi bora kwa watoto ni moja ya jambo la msingi na ndio maana serikali ya Zanzibar imekuwa ikiweka mikakati ya kuwatunza watoto ikiwa ni oja na kuwawekea Idara yao.

Mama Asha aliwataka viongozi, wafanyakazi, watoto na walezi, wa kijiji hicho kuendeleza mshikamano na serikali itahakikisha inakuwa pamoja nao kwa kukindeleza kijiji hicho.

Aidha aliwapongeza wanafunzi wa skuli hiyo kutokana na kufanikiwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka 2010, na kidato cha sita 2011, kwani wameweza kuwa wa kwanza kwa skuli za Zanzibar.

Hata hivyo aliwataka viongozi wa skuli hiyo kufikiria kuwasaidia mbinu bora Wizara ya Elimu waliyotumia ili skuli za serikali  nazo ziweze kupata mafanikio hayo kwa vile Zanzibar ni moja.

Mama Asha aliwakabidhi watoto wa kijiji hicho televisheni tatu zenye thamani ya shilingi milioni 4.5 na vijuzuu pamoja na zawadi nyengine kwa walezi na kuwakabidhi vyeti watumishi wa muda mrefu, ambavyo vimetolewa na yeye binafsi kwa kushirikiana na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein.

Mapema Mkurungezi wa Kijiji hicho, Suleiman Mahmoud Jabir, aliishukuru serikali kwa kukubali kuwa nao pamoja kwa muda wote na kuhakikisha kuwa wataendeleza kutoa malezi mazuri kwa watoto wa kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kijiji hicho Mohammed Baloo, akitoa maelezo yake nae alimpongeza Mama Asha kwa mchango wake anaoutoa katika kukiendeleza kijiji hicho.

Wakitoa shukrani zao wafanyakazi wa kijiji hicho alieleza kuwa watahakikisha wanatekeleza majukumu yao vyema ikiwa ni hatua itayoweza kuchangia kuwapo kwa malezi bora ya watoto wa kijiji hicho.

Sherehe hiyo ilipambambwa na burudani mbali mbali ikiwemo ngoma za utamaduni na michezo ya sarakasi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.