Habari za Punde

WAWAKILISHI KUJADILI BAJETI LEO

·       Spika awataka kuwawakilisha vyema wananchi
Na Mwanajuma Abdi

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, leo wataanza kujadili Bajeti ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Majadiliano hayo yatafanyika ukumbi wa Baraza hilo huko Chukwani, ambapo wajumbe watapata nafasi ya kujadili, kuchangia, kuchambua na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya Bajeti hiyo.

Mbali ya bajeti hiyo wakati wa asubuhi wajumbe wa Baraza hilo wataendelea katika uulizaji maswali na kupatiwa majibu na Mawaziri wa wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kujadiliwa kwa bajeti hiyo inatokana na kuwasilishwa Jumatano iliyopita katika Baraza hilo, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf  Mzee aliwasilisha ikiwa ni mara ya kwanza tokea Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuingia madarakani mwaka jana.

Waziri Omar alipowasilisha hotuba ya bajeti hiyo alisema
Serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 613.08 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na y a maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Bajeti hiyo, imeweka wazi kwamba Serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote, ambapo imekusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.

Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa kuwa ni kipaumbele katika bajeti hiyo ni pamoja na kutekeleza mkakati wa muda wa kati, unaolenga ukuaji wa haraka ambao utahakikisha maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi endelevu na huduma bora kwa ustawi wa jamii.

Kulingana na malengo ya mkakati huo ni kuimarisha huduma za afya, misisitizo zaidi ukilenga katika ununuzi wa vifaa vya hospitali, dawa muhimu pamoja na kuimarisha huduma zinazotolewa na vituo vya afya vya wilaya/mikoa.

Aidha mengine ni kuimarisha elimu kwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati, vifaa vya maabara, vifaa vya kufundishia na kumaliza ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.

Waziri Yussuf alieleza vipaumbele vyengine ni kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora, mbolea na matumizi ya matrekta pamoja na miuondombinu ya kiuchumi kiwani ni kuendeleza miradi ya barabara, umeme katika maeneo ya kilimo na kufanyika tafiti mbali mbali za uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.

Wakati huo huo, Himid Choko kutoka Baraza la Wawakilishi anaripoti kuwa, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, amewahimiza Wajumbe  wa Baraza hilo kuwawakilisha  vyema  wananchi wao  kwa kuwatetea  katika vipaumbele vitakavyowasaidia   kuimarisha hali zao za maisha  kwa upatikanaji wa huduma muhimu   wakati wa kujadili Bajeti ya Serikali.

Amesema Wajumbe wa Baraza hilo ndio dhamana wa kuidhinisha  matumizi ya fedha  za serikali hivyo hawana budi kuhakikisha  kwamba fedha hizo zinaelekezwa  katika  miradi inayolenga  kupunguza  matatizo ya wananchi wenyewe.
Kificho  aisema hayo jana wakati akifunga semina ya kuwajengea uwezo  waheshimiwa Wajumbe wa  Baraza la Wawakilishi kuhusu mchakato na uchambuzi wa Bajeti katika ukumbi wa Zanzibar Ocean View  Kilimani.

Hivyo Kificho amewataka wajumbe hao kuipitia kwa kina Bajeti ya Serikali na hatimae  kuichambua na kuijadili   katika maeneo yote  hasa yale  yanayogusa utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Nae mkufunzi kutoka chuo cha  Utawala wa  fedha  Chwaka Said Mohammed  Khamis akitoa mada kuhusiana na  Uchambuzi wa Bajeti ya Serikali,  amesema ni muhimu kwa wajumbe hao kutambua  viashiria vya  uchumi  kama vile Pato la Taifa, Mabadiliko ya Bei za Bidhaa na Huduma, Hali ya Ajira  Nchini, urari wa mapato na matumizi ya Nchi  na hali ya Biashara nchini ili waweze kuijadili vyema Bajeti hiyo.

Aidha  Said amesema mbinu nyengine ya uchambuzi wa bajeti ni  kuzingatia sera za kifedha na kodi  ambazo huwa zinatumika kudhibiti  mzunguko wa fedha ambao unaathiri katika uchumi pamoja na kutathmini mwenendo mzima wa ukusanyaji wa mapato .

Akiwasilisha mada juu ya mchakato na changamoto za bajeti Mtaalamu kutoka Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo amesema  Zanzibar kama nchi nyengine zinazoendelea inakabiliwa na changamoto  kadhaa ikiwemo Vyanzo vidogo vya kodi, kasi ya ukuaji wa utalii usiolingana na na kasi ya ukuaji wa mapato yanayotokana na utalii huo pamoja na mahitaji makubwa ya rasilimali fedha  kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali kama ilivyoelekezwa katika Mpango mkuu wa  wa kupunguza umasikini hapa nchini.

Ameongeza kwamba changamoto nyengine inayoikabili  Bajeti ya Zanzibar ni kiwango kikubwa cha utegemezi wa  wahisani  pamoja na shinikizo  la kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na kiwango kidogo cha fedha za ndani  kwa matumizi ya  miradi ya maendeleo.

Nae Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee Ibrahim, amewahimiza  wajumbe hao kuzingatia kanuni za majadiliano  ya Kibunge huku wakitilia mkazo  hoja inayohusika  pamoja na kuwatetea wananchi wao.

Semina hiyo  ya siku moja imeandaliwa kwa pamoja na Ofisi ya Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na  Ofisi ya Raisi, Fedha, Uchumi na Mipango ya maendeleo ikiwa ni miongoni mwa juhudu za kuwajengea Uwezo wawakilishi ambao mara nyingi wao sio wataalamu wenye  elimu  na ujuzi  wa masuala ya fedha na uchumi ingawa kwa mujibu wa Katiba ndio wenye kazi ya kujadili na kupitisha bajeti ya serikali.

Bajeti ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 20011/2012 iliwasilishwa Jumatano iliyopita na leo inaaza kujadiliwa  katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.