Habari za Punde

BAJETI YA ELIMU YAPITA

Na Mwandishi wetu

HATIMAE Baraza la Wawakilishi limeipitisha bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) baada ya vuta nikuvute kati ya Wawakilishi na Waziri wa wizara hiyo.

Lakini bajeti hiyo ililazimika kupitishwa kifungu kwa kifungu kama zilivyokuwa bajeti za Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano.

Bajeti hiyo imepita baada ya Waziri Ramadhan Abadalla Shabaan kuweza kujibu hoja zilizojengwa na Wawakilishi kwa baadhi ya Idara, wakiwemo,Ismail Jusa Ladhu, Rashid Seif, Mohamed Said, Subeit Khamis Faki na Saleh Nassor Juma.

Pamoja na mambo mengine wawakilishi hao walihoji kuhusiana na masuala ya Mfuko wa elimu ya juu Zanzibar, wajumbe wa Zanzibar waliomo katika

Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu Tanzania, uchache wa wanafunzi wa elimu ya juu wanaofaidika na mikopo kutoka mfuko wa elimu ya juu Zanzibar.

Masuala mengine ni kiwanja kilichotolewa na serikali kwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), mradi wa mafunzo ya ualimu, maabara na Idara ya elimu ya sekondari.

Akijibu hoja ya wajumbe wa Zanzibar waliomo katika bodi ya mfuko wa elimu ya juu Tanzania (HESLB) Waziri Shaaban alisema bodi yote ina wajumbe 14 kati yao wanne wanatoka Zanzibar.

Aidha kuhusu Necta, Waziri Shaaban alisema serikali iliipatia kiwanja baraza hilo na yeye wakati huo akikaimu ofisi ya Waziri Kiongozi, ndiye aliyeikabidhi Necta hati ya umiliki wa kiwanja hicho, lakini walishindwa kukiendeleza.

Alisema baada ya miaka isiyopungua minne tokea hati hiyo kutolewa huku kiwanja hicho kikiwa hakijaendelezwa, Wizara ya Fedha ilifuta hati hiyo na kuipatia Wizara ya Mawasiliano kwa ajili ya kujenga ofisi zake.

Kupita kwa wizara hiyo sasa kunaifanya Wizara ya Elimu kuruhusiwa kutumia shilingi 102,618,054,000 katika makisio yake kwa matumizi ya mwaka wa fedha 2011/2012.

Kati ya fedha hizo, shilingi 45,308,000,000 zitatumika kwa matumizi ya kawaida na shilingi 57,310,054,000 kwa kazi za maendeleo.

Awali akiwasilisha makisio ya bajeti ya wizara yake, Waziri Shabaan aliahidi kuwa atachukua juhudi kupambana na na mimba za utotoni, ndoa za mapema kwa wanafunzi na dawa za kulevya.

Aidha skuli mpya 16 za sekondari zitafunguliwa katika mwaka huu wa fedha pamoja na kuongeza walimu wenye sifa wa masomo ya Sayansi, sambamba na kuongeza idadi ya vitabu na vifaa vya maabara.

Pia aliahidi kutokomeza maradhi ya kichocho kwa wanafunzi kwa ushirikiano na Wizara ya Afya.

Leo Wawakilishi wanaendelea kuijadili bajeti ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.