Habari za Punde

MAALIM SEIF APIGA MARUFUKU UPASUAJI MIAMBA

Na Abdi Shamnah
 MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wananchi wa shehiya ya Sanani Muwambe kuacha mara shughuli za upasuaji miamba kwa ajili ya matofali, vinginevyo watakumbana na rungu la Dola.

 Maalim Seif ametoa indhari hiyo huko Muwambe alikofika kuona utekelezaji wa maagizo ya Serikali, yanayowataka wananchi hao kuachana na kazi hizo zenye kuleta uharibifu mkubwa wa mazingira, huku Serikali ikitafuta shughuli mbadala ili waweze kujikimu na maisha.
 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilipiga marufuku shughuli za upasuaji miamba kwa ajili ya matofali, na kuitaka Wizara ya Kazi, Ajira na Uwezeshaji wananchi kiuchumi kutafuta shughuli mbadala kwa wananchi hao, ambapo vikundi 18 tayari vimeshasajiliwa kwa ajili ya kupatiwa miradi.
Amesema Serikali haina nia ya kumuonea mtu yeyote, lakini iko macho kulinda sheria za nchi na kuhifadhi mazingira yake, hivyo mtu yeyote atakaepatikana kuhusika na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali.
 Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkoani kushirikiana na sheha wa Shehiya hiyo pamoja na wananchi kuona tatizo hilo linaondoka kabisa kwa maslahi ya Taifa na kizazi chao.
 Alisema vitendo vya upasuaji wa miamba kwa ajili ya matofali vina athari kubwa kwa wananchi wenyewe kwa kuzingatia mashimo hayo makubwa yamezunguka nyumba zao na kuhatarisha maisha ya watoto wadogo au wageni wanaowatembelea.
 Maalim Seif alisema serikali ina mipango thabiti na ahadi yake ya kuwatafutia wananchi wa kijiji hicho njia mbadala za kimaisha ipo pale pale.
Alisema yeye binafsi atalifuatilia kwa karibu suala hilo, ili kuhakikisha Serikali kupitia Wizara ya Kazi,Ajira na Uwezeshaji wananchi kiuchumi inafanya juhudi za haraka na kuvipatia miradi vikundi vilivyoundwa.
 Alisema serikali inafahamu kuwa kwa miaka mingi wananchi wa Mwambe wamekuwa wakifanya shughuli za kuchimba matofali, lakini haiwezi kuendelea kuruhusu kwa hofu ya ardhi iliopo kumalizika.
 Aliwakumbusha wananchi hao kuwa Zanzibar ni kisiwa, hivyo watu wote  wana wajibu wa kushirikiana na Serikali kuitunza ardhi  ndogo iliopo kwa faida ya kizazi kijacho.
 Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa
Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkoani kuwafikisha mahakamani watu wote watakaopatikana kuhusika na vitendo vya uchongaji wa matofali katika kijiji hicho.
 Alisema ofisi yake itafuatilia kwa karibu kuona vitendo hivyo vinasita mara moja, sambamba na upatikanaji wa shughuli mbadala kwa wananchi wa kijiji hicho.
 Katika hatua nyingine Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amebariki marufuku iliotolewa na Idara ya Mazingira ya kukataza uchongaji wa matofali karibu kabisa na Mnara wa Ras Kigomasha.
Amelitaka jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kusaidia ulinzi katika maeneo hayo baada ya kubaini, kuwepo wananchi toka maeneo jirani wanaoendesha vitendo vya uchongaji wa matofali hayo nyakati za usiku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.