Wananchi kushuhudia halua ikisongwa 'live'
Na Salum Vuai, Maelezo
MAONESHO ya siku tano ya utamadani wa taifa la Oman, yanatarajiwa kufunguliwa leo katika jengo la kihistoria Beit El Ajaib, Forodhani mjini hapa.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Wizara ya Urithi na Utamaduni ya nchi hiyo, linajumuisha mambo mbalimbali ya kiutamaduni wa asili ya Oman, zikiwemo ngoma, filamu, semina na mijadala kuhusiana na mambo ya utamaduni zitakazofanyika Julai 14 na 15 katika jumba la Makumbusho ya Kasri Forodhani.
Kwa mujibu wa Balozi huyo, kutakuwa na watoaji mada kadhaa kutoka Oman na Zanzibar watakaotoa somo la mambo ya utamaduni wa Oman na historia yao katika nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mnazimmoja, Balozi Mdogo wa Oman Majid Abdallah Al Abadi, alisema pamoja na mambo mengine, tamasha hilo linalenga kuwaleta karibu wananchi wa nchi yake na Zanzibar katika harakati za kuendeleza uhusiano wa miaka mingi baina yao.
Al Abadi alisema pamoja na shughuli hiyo kuanza tangu saa tatu asubuhi katika jengo la Beit El Ajaib, ufunguzi rasmi utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana na baadae saa moja jioni kutakuwa na maonesho ya ngoma, filamu na mavazi yenye asili ya Oman. katika ukumbi wa Ngome Kongwe.
Kwa siku zote za tamasha hilo, mambo mbalimbali yataoneshwa katika Beit El Ajaib ikiwemo sebule ya Kiomani, kazi za mikono kama kuchonga majahazi, nyaraka za kihistoria na vitabu tafauti, usongaji halua na upishi wa kahawa ambapo wananchi watapata fursa ya kushuhudia na kuonja, huku maonesho ya Ngome Kongwe yakiendelea kurindima.
Aidha, Balozi Al Abadi alisema sanaa ya uchoraji hina kwa wanawake wa Kiomani itakuwepo sambamba na kuandika hati za Kiarabu kwa mkono ambapo pia watakaotaka kuandikiwa maandishi maalumu watafaidika.
Alifahamisha kuwa, kwa kawaida Oman huendesha tamasha hilo katika nchi mbili ziliko ofisi zake za ubalozi, ambapo mwaka jana yalifanyika China na Japan, na mwaka huu imeamuliwa yafanyike Zanzibar pamoja na Australia.
Alisema tukio hilo, linalenga kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya Oman na Zanzibar kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa ushirikiano uliosainiwa kati ya nchi hizo Agosti 17, 2010.
"Hili ni jambo adhimu kwetu, nchi zetu zinafanana kwa mengi ukiwemo utamnaduni hasa kutokana na historia ya kuwepo Waomani kwa miaka mingi iliyopita, hali iliyowafanya watu wetu wajenge uhusiano na udugu wa karibu", alisema.
Alishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikino na msaada wake iliotoa katika kufanikisha tamasha hilo, na kuwataka wananchi wafike kwa wingi na kwamba hakutakuwa na kiinglio cha fedha.
Naye Kamishna wa Michezo na Utamaduni Hamad Bakari Mshindo, alieleza kufurahishwa na hatua hiyo, na kusema ni muhimu kwa kukuza mafahamiano na ushrikiano katika nyanja mbalimbali za kijamii na maendeleo kwa jumla.
No comments:
Post a Comment