Habari za Punde

SOKA ZANZIBAR KUENDELEA KUCHEZWA KORTINI

New Boko kuipandisha kizimbani kamati ya rufaa ZFA

Na Donisya Thomas

ANGA la soka Zanzibar, linazidi kuandamwa na mikosi, huku baadhi ya klabu zinazodai kutotendewa haki na chama cha mchezo huo (ZFA), zikiamua kuisaka katika viriri vya mahakama.


Wakati klabu ya Dynamo ikitishia kuishtaki  ZFA Wilaya ya Mjini kwa madai ya kuhujumu  fedha za chama hicho, timu ya New Boko inayoshiriki ligi daraja la pili taifa, nayo imetangaza dhamira ya kuifungulia kesi  kamati ya rufaa na usuluhishi ya chama hicho, ikiishutumu kutoa maamuzi bila kufuata kanuni za soka.

Uamuzi huo umekuja kufuatia kamati hiyo kuamuru timu ya Kijichi Stars ipewe ushindi wa magoli mawili na pointi tatu baada ya kubainika kuwa New Boko ilimchezesha mchezaji Said Khamis Ndemla bila kuzingatia sheria za usajili.

Akizungumza na gazeti hili, Rais wa New Boko Abdi Ali 'Mrope', alisema timu yake ina kila haki ya kumtumia mchezaji huyo kwa kuwa imemsajili kihalali na kwamba ni mali yake.

Alifahamisha kuwa, timu yake ilimsajili Ndemla kutoka klabu ya Mapipa Rangers ya  Dar es Salaam tarehe 14 Mei, 2010 na kuidhinishwa na Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (KIFA), kilichotoa kibali kilichoonesha kuwa mwanasoka huyo ni huru na anaweza kuichezea New Boko.

Kuthibitisha kauli yake, Mrope alilionesha gazeti hili barua iliyotolewa na KIFA iliyoandikwa Mei 14, 2010 yenye kumbukumbu namba KIFA/GF/VOL.111/177/2010, iliyoeleza kuwa  mchezaji Said Khamis Ndemla ni huru na New Boko kupewa mamlaka ya kumtumia katika michezo yake.

Kutokana na barua hiyo, Mrope alisema  hakuna sababu kwa kamati ya rufaa na usuluhishi kuipa ushindi Kijichi Stars na kumfungia mchezaji huyo kutocheza mpira kwa muda wa mwaka mmoja.

Alihoji uhalali wa hukumu ya kamati hiyo dhidi ya timu yake, huku akinukuu kifungu namba 7 (g) cha kanuni za usajili na uhamisho, kinachoeleza kuwa, ili mchezaji kutoka Tanzania Bara aweze kusajiliwa na timu ya Zanzibar, ni lazima ipatikane barua kutoka timu anayohamishwa, kitu alichosema New Boko ilitekeleza.

Kutokana na sakata hilo, New Boko imetoa wiki moja kwa kamati ya rufaa na usuluhishi kutengua maamuzi yake, vyenginevyo  italipeleka suala hilo mahakamani ili kutetea haki yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.