Wanawake wa kizungu wawang’ang’nia, wawachukua Ulaya
Na Mwanajuma Abdi
HAMKANI imeskuwa si shuwari katika kijiji cha Kiwengwa baada ya wanaume wa kabila la Kimasai kuvuruga na kuvunja ndoa za watalii wanaoingia katika kijiji hicho.
Akizungumza na gazeti hili huko Kiwengwa mkoa wa Kaskazini, Sheha wa hiyo Maulid Masoud Unguja alithibitisha kuwepo kwa taarifa za wazungu wanaolalamikia kuibiwa wake zao na wanaume wa Kimasaii.
Alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo, kuna kesi tano zilizoripotiwa na wazungu wa kiume kukimbiwa na wake zao na kuhamia kwa wamasai, huku wageni hao wakiwa ni wanandoa.
Alieleza wamasai katika kijiji hicho wamepata soko kwa wazungu wa kike, ambao wengi wao wanavunja ndoa zao, hali inayosababisha wazungu wa kiume kusambaza ujumbe kwa njia ya mtandao kuwatahadharisha wenzao juu ya wimbi hilo.
Alifahamisha kuwa, Kiwengwa hivi sasa kuna idadi kubwa ya wamasai, ambao wamekuwa wajipatia pato hilo kwa kuiba wake wa wazungu huku kukiwa na taarifa kuwa wabo baadhi yao tayari wameshachukuliwa na wanawake wa kizungu nje ya nchi.
Aidha alisema wimbi hilo haliwezi kuondoshwa kwa vile katiba ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar imeweka wazi raia wa Tanzania anauhuru wa kuishi mahali popote hivyo inakuwa vigumu kwa vile hawaleti madhara katika kijiji hicho.
Nao wananchi mbali mbali wanaojishughulisha na biashara za kitalii katika fukwe za Kiwengwa, walikiri kwamba wamasai wamepanda chati hali inayosababisha hata wanaume wa kiswahili kuingia wivu.
Walisema mbali ya kuchukuliwa lakini pia wamekuwa na mvuto katika biashara wanazozifanya, jambo ambalo kwa watu wengine waliokuwa sio kabila la wamasai huuza kwa tabu.
Walifahamisha kuwa, maisha yamekuwa magumu kutokana na wazungu kukimbilia katika mabanda ya wamasai.
Kiwengwa inajumuisha vijiji vitatu vya Cairo, Kumba Urembo na Gulioni, ambavyo vina jumla ya wakaazi 2,500 kati ya hao 50 wamefaidika na ajira rasmi ya hoteli za kitalii na wavuvi, wanaendesha biashara wenyewe zikiwemo za utalii na kazi mbali mbali.
No comments:
Post a Comment