

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkurugenzi wa Skuli ya Mbarali Bw, Ali Pandu Haji shilingi Milioni moja na nusu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitowa wakati wa maadhimisho ya miaka kumi tokea kuanzishwa kwa skuli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema mchango unaoendelea kutolewa na skuli binafsi umewezesha kuisaidia serikali kwa kiwango kikubwa katika kupunguza mzigo wa kuwahudumia wanafunzi maskulini.
Balozi seif amesema hayo hapo Afisini kwake Vuga wakati akikabidhi shilingi milioni moja na nusu kwa uongozi wa skuli ya Mbarali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitowa wakati wa maadhamimisho ya miaka kumi tokea kuanzishwa kwa skuli hiyo.
Fedha hizo ni ahadi ya kwanza miongoni mwa alizoahidi tarehe 16/7/2011 kusaidia madeski ya darasaa moja, kompyuta moja, milioni moja kusaidia ununuzi wa madaftari, na shilingi laki tano kwa vikundi vya wanamichezo na wasanii waliotumbuiza siku ya sherehe hiyo.
Balozi Seif amesema sekta ya elimu nchini hivi sasa ni ya kuridhisha kutokana na mchango huo wa skuli binafsi licha ya changamoto zinazoikabili serikali katika ukamilishaji wa baadhi ya vifaa.
Amesema Skuli nyingi bado hazijawa na madeski na juhudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na taasisi na mashirika ya maendeleo.
“ Kima cha Madeski kwa Skuli zote za Unguja na Pemba kimekadiriwa kuwa Madeski 35.000 kiwango ambacho bado ni changamoto kwa Serikali ”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif ameainisha kwamba Serikali bado inaendelea kukabiliana na kazi kubwa ya kuzijengea uwezo wa Kimaabara skuli zake kwa lengo la kuimarisha Somo la Sayansi.
Amesema hatua hiyo inakusudia kuongeza kiwango cha wanafunzi wa fani hiyo ambayo bado iko chini hasa ikilinganishwa na ukuaji wa sayansi na teknolojia uliopo Duniani hivi sasa.
Amesema mazingira hayo yatawapa fursa Vijana kufikia lengo la kuwa wataalamu mahiri wa Taifa hapo baadaye.
Akipokea msaada huo Mkurugenzi wa Skuli ya Mbarali Bwana Ali Pandu Haji amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa Juhudi zake za kusaidia Skuli Binafsi.
Bwana Pandu amesema katika kuunga Mkono juhudi za Serikali Uongozi wa Skuli ya Mbarali umeweka Kiwango kidogo cha ada ya wanafunzi ili kumuwezesha kila mtoto anapata Haki yake ya Elimu na msingi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Ni jambo la maana,na sisi wazanzibari tuamke ktk kuchangia masuala ya elimu.kwa kweli tumelala mno! inaonekana kitendo cha karume kutangaza elimu bure visiwani mwaka 1964 kilitupumbaza.huwezi kuamini lakn. z.nz. hata mtu akiwa na kipato cha mil.20 kwa mwezi utakuta mwananawe anasoma skuli ya serekali na wala hachangii chochote! kubwa anaweza akalaumu serekali kama mtoto wake atatakiwa kuchangia chochote utasikia 'hii ndio elimu bure kweli'matokeo yake wizara imeelemewa kiuchumi,watoto wengi,madarasa kidogo,mishahara ya waalimu haitambuliki,hatimae viwango duni vya elimu. hujui aliyesoma wala asiesoma mawazo ya ajaabu!
ReplyDelete