Habari za Punde

MAAALIM SEIF: ITIKADI ZIWE DARAJA LA MAENDELEO

Akemea kugeuka vurugu, chuki, uhasama

Abashiri serikali ya Umoja Bara

Na Hassan Hamad (OMKR), Tabora

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, maalim Seif Sharif Hamad amesema itikadi za kisiasa ni daraja la kufikia maendeleo ya wananchi na sio chanzo cha vurugu, ugomvi wala uhasama miongoni mwa jamii.


Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema kwamba vyama vya siasa vitaendelea kutafautiana kisera, kiitikadi na kiilani, lakini viongozi lazima waelewe kwamba lengo ni kuleta maisha bora ya wananchi na siyo mifarakano na ugomvi baina yao.

Maalim Seif alieleza hayo huko Urambo, mkoani Tabora katika zaiara yake iliyofuatia mwaliko wa viongozi wa CUF mkoani humo kufungua miradi ya maendeleo kuzungumza na wananchi pamoja na kupata taarifa za utendaji wa chama hicho.

Alisema vyama vya siasa vinaweza kufanya shughuli zao bila ya kusababisha vurugu hali ambayo tayari imethibitika Zanzibar baada ya wananchi kuamua kuuzika uhasama wa kisasa na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Alisema pamoja na kuwepo vyama vingi vyenye itikadi tafauti kama vile CCM na CUF Zanzibar, lakini kwa sababu vimeamua kuweka mbele maslahi ya wananchi mafanikio makubwa yameanza kupatikana Zanzibar chini ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Alifahamisha kuwa muda mfupi tangu kuundwa serikali hiyo Zanzibar, dalili za mafanikio makubwa zimeanza kuonekana ikiwemo za kisiasa na kiuchumi hali ambayo itastawisha maisha ya wananchi.

Akitoa mfano alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo umoja wa kitaifa Zanzibar imeweza kusimamia bei ya zao la karafuu na sasa wakulima wa zao hilo wanaliuza kwa bei ya kuridhisha.

Alisema awali kilo moja ya karafuu ilikuwa ikiuzwa shilingi 5,000, lakini msimu huu zimepandishwa bei mara kadhaa na hivi sasa wakulima wanauza kilo moja shilingi 15,000.

Alieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uamuzi wa serikali kuwawezesha wakulima wanufaike na asilimia 80 ya bei ya mazao yao kwa bei ya soko la dunia.

Alifafanua hali hiyo imeleta ari kubwa kwa wakulima wa zao hilo ambao sasa wanaitunza na kuipanda kwa wingi mikarafuu, baada ya huko nyuma kuitelekeza kutokana na bei kuwa ya chini.

Alieleza hivi sasa kila chama kinachangia maendeleo lengo likiwa ni kuinua maisha ya wananchi angalau kwa kuanzia kila mwananchi amudu dola mbili kwa siku katika kujinasua na ugumu wa maisha, mipango ambayo alisema inawezekana wananchi wakiamua kufanya kazi kwa bidii.

Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema mafanikio yanayoonekana Zanzibar hivi sasa ni makubwa, kwa sababu hapo awali kila baada uchaguzi mkuu wananchi walikuwa na hofu ya kukumbwa na vipigo na uhasama miongoni mwao.

Alisema wananchi watakapoweka kando uhasama wa kisiasa wataweza kuungana na kupata mafanikio makubwa katika kuzitumia rasilimali nyingi zilizopo kwa manufaa ya Watanzania wote.

“Zanzibar ni kama maabara, mambo yote yanaanzia Zanzibar, naamini serikali ya umoja wa kitaifa itakuja na Tanzania Bara” alisema Maalim Seif huku akishangrliwa na wanaCUF pamoja na wananchi waliojitokeza katika mkutano huo.

Maalim Seif alisema Mwenyezi Mungu ameijaalia Tanzania kuwa na maliasili nyingi ikiwemo madini ya kila aina, ardhi yenye rutuba na hali ya hewa safi, hivyo ni jukumu la watanzania kuzitumia rasilimali hizo na kuwanufaisha wananchi.

Katika zaira hiyo aliweka mawe ya msingi katika Ofisi ya serikali ya kijiji cha Ushokola, Usinge na kwenye nyumba ya mganga (daktari) katika kijiji cha Usinge, sambamba na kuahidi kuchangia shilingi milioni mbili na nusu kwa ajili ya kusaidia kumalizia ujenzi wa tawi la CUF katika kijiji cha Ushokola.
Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Tabora, Maalim Seif aliambatana na Mkuu wa Mkoa huo, Abeid Mwinyi Mussa, Mkuu wa wilaya ya Urambo, Anna Magoa pamoja na maofisa wa chama cha CUF katika mkoa huo.

Maalim Seif jana aliwasili jimboni Igunga mkoani Tabora, kushiriki kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo hilo.

Vyama sita vya siasa vinashiriki katika uchaguzi huo, ambavyo ni CCM,CUF, CHADEMA, Sauti ya Umma, UMD na DP.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.