Habari za Punde

TAARIFA YA WIZARA YA AFYA ZANZIBAR KUHUSU AJALI YA MELI


KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohammed Jidawi, akizungumzia juu ya hali za majeruhi baada ya kufikisha katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, alisema wengi waliweza kupatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.

Alisema hali ya upatikanaji wa dawa kwa majeruhi ambao walilazimika kulazwa katika Hospitali hiyo alisema sio mbaya kutokana na wengi wa wagonjwa hao hawakuwa na majeraha makubwa.

Alisema sehemu kubwa ya wagonjwa hao walikuwa wamepatwa na mshutuko jambo ambalo limewasababishia kupoteza fahamu.


Alisema sehemu kubwa ya madaktari wameweza kuitikia wito wa kuingia kazini na kutoa huduma kwa wakati ambapo Katibu huyo aliwapongeza.

Aidha, alieleza kuwa tayari kuna mashirika mbali mbali ya kimataifa ikiwemo WHO limewapatia misaada ya dawa tofauti pamoja na baadhi ya Wafanyabishara akiwemo Mfanyabiashara Mohammed Saleh Baharesa na Muzamil.

Hata hivyo alisema tayari serikali ya Muungano kupitia Wizara ya Afya imeahidi kutoa madaktari kuja kusaidia kuwapatia huduma wagonjwa wataokuwa na hali mbaya.

UOKOZI
MSIMAMIZI wa uokozi katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islander 1, SGR Hussein Mohammed Hussein, aliiambia Zanzibar Leo kazi ya uokozi wa maiti hizo iliweza kufanyika vizuri kutokana na kupata msaada mkubwa wa kuyafikia maeneo baada ya kutumia Helikopta.

Alisema uwezekano wa kupatikana maiti zaidi unaweza kuwepo kutokana na sehemu kubwa ya maiti zilizookolewa ni zile zilizoweza kutoka kabla ya meli hiyo kuzama.

Hata hivyo alisema sehemu kubwa ya wahanga wa ajali hiyo walijitahidi kujiokoa baada kutumia vitu mbali mbali yakiwemo magororo na baadhi ya vifaa vigumu.

VIKOSI

VIKOSI vya Ulinzi na Usalama, vimefanikiwa kudhibiti kutokea hali zote za vurumai katika maeneo yote ya Mji wa Zanzibar huku wakitoa msaada mkubwa wa kubeba majeruhi na waliofariki na kuwafikisha maeneo husika.

Aidha, vikosi hiyo pia vilionekana kuwa na wakati mgumu baada ya umati wa watu kutaka kuvamia eneo la utoaji maiti ili waondoke nazo baada ya kutakiwa kufuata utaratibu.


WALIOOKOKA
Baadhi ya waliookoka baada ya kupatiwa matibabu walieleza hali zao zimerudi katika ukawaida lakini wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu madogo madogo.

Mtoto wa miaka mitano Aiman Idiria alisema baada ya kupata matibabu yuko salama kutokana na kupata maumivu baada ya wakati akijiokoa baada ya kupanda polo hadi walipofika waokozi.

Majeruhi mwengine Mohammed Mussa, alisema hali ilikuwa mbaya kabla ya kuokolewa kutokana na kuchukua muda mrefu kung’ang’ania kamba na boya hadi alipookolewa.

Alisema wakiwa katika meli hiyo waliwaona mabaharia wakihangaika kuchukua ndoo na kutoa maji na walipojaribu kuwauliza kinachoendelea waliwaahidi kuwa wapo salama.

Hata hivyo baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya waliamua kujitosa baharini na ndipo alipopata kamba hiyo na kulazimika kujiokoa ambapo alieleza watu walikuwa ni wengi kwani walikaa hadi katika vyoo.

Dk. kutoka Cuba, Luckman Isie, ambae alikuwa dhamana wa maiti kiwanja cha Maisara, alisema watoto wengi walipatikana wamekufa wakiwa wamegandana na mama yao, hivyo ilikuwa vigumu kuwatenganisha.

MAKAMPUNI YA MELI

Makampuni ya Meli jana asubuhi yalilazimika kuvunja safari zao na kujitolea kushiriki katika zoezi ambapo meli ya See Bus II na Express zilifanya kazi ya kubeba majeruhi waliopatikana pamoja na maiti.

Meli nyengine ambazo zilishiriki katika uokozi huo ni pamoja na ya Vikosi vya KMKM ikiwemo MISALI na meli ya Serengeti.

HUDUMA YA KWANZA

VIKOSI vya Msalaba Mwekundu wakati wa tukio hilo vilitoa huduma hizo katika bandari ya Zanzibar ambapo mama mmoja baada ya kuokolewa alizirai baada ya kufika juu huku wakilazimika kutoa msaada mkubwa wa vifaa.

RAIA WA KIGENI

Baadhi ya majeruhi ambao walilazimika kupata huduma katika tukio hilo walikuwemo na raia wa kigeni ambao bado hawakujulikana utaifa wao.

BANDARI

WATENDAJI wa shirika la Bandari wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mustafa Aboud Jumbe, walionekana kuwa na wakati mgumu baada ya majeruhi hao kufika salama.

Hali hiyo ilisababishwa na umati wa watu kufika kutaka kutambua maiti zao huku wakilazimika kuwapatia msaada wa dharura kabla ya kufikishwa katika Hospitali kupatiwa matibabu.

Hata hivyo vilio vilisikika kutawala zaidi kwa baadhi ya majeruhi kufika katika bandari hicho kwa kutoamini kwamba wamenusurika kupoteza maisha yao.

MABALOZI

WATENDAJI katika Afisi za Kibalozi na Watendaji wa Mashirika ya Kimataifa ya nchi mbali mbali waliokuwapo nchini Tanzania, jana jioni walitoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Balozi wa Uingereza nchini Diane Corner, Kamishana Mkuu katika Ubalozi wa Uingereza alimueleza Dk. Shein kuwa serikali yao imeguswa na tukio hilo na kuwatakia pole wazanzibari wote.

SPIKA

KUTOKANA na kuwapo kwa msiba huo Baraza la Wawakilishi limeakhirisha ziara iliyokuwa inafanya Mkoani Arusha kwa muda wa siku nne.

Wengi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nao walijotokeza kwa kutoa misaada mbali mbali kwa jamii wakati wa kuzitambua maiti hizo.

WANANCHI
Wananchi wa Zanzibar waliojitokeza katika kushuhudia tukio hilo walijitolea kufanya kazi mbali mbali za dharura ikiwemo za kuosha maiti pamoja na kuvisha sanda.

OFISI
Baadhi ya taasisi za kuhudumia vifo walilazimia kuhamia katika viwanja vya Maisara ya kuendesha utoaji wa huduma ikiwemo ya vizazi na vifo, huku masheikh na baadhi ya Jumuiya za kujitolea za kidini kushiriki kutoa huduma mbali mbali ikiwemo Jumuiya ya Uamsho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.