Habari za Punde

MAALIM SEIF AZIKOROMEA TAKUKURU, OFISI YA MSAJILI

Amtaka Msajili asaidie wananchi wapate Vitambulisho Z’bar

Na Khamis Haji, OMKR

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka ofisi ya Msajili wa vyma vya Siasa nchini na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyotungwa nchini inafuatwa na kutekelezwa kivitendo, ili chaguzi zinazofanyika ziwe huru na haki na zisizotawaliwa na rushwa.

Maalim Seif alisema hayo jana huko Makao Makuu ya CUF Zanzibar mtaa wa Mtendeni, wakati alipotembelewa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Rajab Baraka katika ziara yake ya kawaida ya kuvitembelea vyama hivyo.


Alisema pamoja na kutungwa sheria hiyo, baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikiikiuka hadharani, kwa kutoa rushwa bila kificho pamoja na kukiuka kima kilichowekwa cha gharama za uchaguzi wa jimbo, bila ya kuchukuliwa hatua zozote na Mamlaka husika.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitoa mfano wa ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo ni ni matukio yaliyojiri wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga, mkoani Tabora mwezi Septemba mwaka huu.

Alieleza kuwa wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga sheria ya Gharama za Uchaguzi ilifumbiwa macho, kwasababu licha ya sheria hiyo kuweka bayana kima cha juu cha gharama za uchaguzi wa jimbo kisizidii shilingi milioni 80, kuna chama kilitangaza kwenye vyombo vya habari kitatumia shilingi milioni 400 katika uchaguzi huo.

“Yaliyotokea Igunga ni uthibitisho wa ukiukwaji wa sheria hii, rushwa ilikuwa ikitolewa nje nje, TAKUKURU wapo wanaona, sasa kama tumeamua kutunga sheria basi tuzifuate sote”, Maalim Seif alimueleza Naibu Msajili wa vyama.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif ameitaka ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwasaidia wananchi wanaokosa haki zao kwa kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, kwa kuzishitua mamlaka zinazowawekea vikwazo wananchi hao ziache tabia hiyo, kwasababu ni kuwanyima haki zao na kuleta ubaguzi miongoni mwa wananchi.

Alimueleza Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa hivi sasa kuna wananchi wengi wa Zanzibar wanazunguushwa na kukoseshwa fomu za kuomba vitambulisho hivyo, kwasababu za kisiasa, hali inayowasababishia wakose haki zao nyingi za msingi, mbali na shughuli za uchaguzi.

“Nashindwa kufahamu hawa Masheha, Maafisa Wilaya na wa Idara ya Vitambulisho vya Ukaazi wana uzalendo kweli na Zanzibar”, alihoji Maalim Seif.

Alieleza kwamba kwa bahati mbaya sana vitendo hivyo vya kuwanyima Wazanzibari vitambulisho vya Ukaazi vinaendelezwa hata wakati huu, ambapo nchi inaelekea kwenye mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kwamba kitambulisho hicho kitahitajika kumjua Mzanzibari, ili aweze kupata haki ya kutoa maoni yake juu ya Katiba mpya.

Maalim Seif alisema wakati wananchi hao wa Zanzibar wakinyimwa vitambulisho hivyo, wapo vijana kutoka Tanzania Bara wamekuwa wakipatiwa vitambulisho hivyo, kwa urahisi licha ya kuwa kwa mujibu wa sheria wahastahili kupewa.
Naibu Msajili huyo wa Vyama vya siasa alisema amesikia malalamiko hayo na atayafanyia kazi, kwania ya kuinua hali ya demokrasia nchini.

Alivitaka vyama vya siasa ambavyo havifanyi kazi zake ipasavyo, na kusubiri wakati wa uchaguzi, kama vile kuitisha vikao kwa mujibu wa sheria, viache tabia hiyo kwasababu haisaidii kukuza uhai wa vyama na pia inadumaza demokrasia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.