Habari za Punde

MIEMBENI UNITED YACHANJA MBUGA LIGI YA SEAGULL

Na Mwajuma Juma

TIMU ya soka ya Miembeni United imeendelea kutesa katika Ligi Kuu ya Seagull ya Zanzibar baada ya kuifunga Chuoni goli 1-0. Mchezo huo ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Dzedong mjini hapa.

Kwa ushindi huo, Miembeni United imeweza kufikisha pointi tisa baada ya kushuka dimbani mara tatu na kushinda michezo yote.


Miembeni United ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Zanzibar Ocean, ilionekana kuwazidi wapinzani wao katika kila idara na kufanikiwa kupata goli hilo pekee katika dakika ya 50 ya mchezo huo.

Shujaa wa miamba hiyo alikuwa mshambuliaji Suleiman Ali ‘Pochori’ ambaye aliunganisha pasi safi ya Issa Othman ‘Amasha’.

Hicho kilikuwa kipigo cha pili kwa Chuoni ambayo katika mchezo uliopita ilifungwa pia goli 1-0 na Kikwajuni hapo Novemba 24.

Hata hivyo katika mchezo huo Chuoni iliyokuwa ikicheza chini ya kiwango itapaswa kujilaumu pale mchezaji wake, Abdul Kapenta, alipoikosesha timu yake goli la kusawazisha katika dakika ya 80, kufuatia kupiga shuti lililogonga mwamba na mpira huo kuokolewa na walinzi wa Miembeni United.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo uwanjani hapo kwa mchezo mkali utakaowakutanisha maafande wa Polisi na Miembeni SC, timu zote zikiwa na majeraha ya kufungwa na Miembeni United katika michezo yao ya awali.

Jumla ya timu 12 zinashiriki ligi hiyo ambapo bingwa atapata shilingi milioni 10 na mshindi wa pili milioni tano wakati mshindi wa tatu atapata shilingi milioni tatu, huku mchezaji bora akiondoka na vespa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.