Habari za Punde

CENTRAL YAANDAA ABEID KARUME MAPINDUZI CUP

Yatashirikisha kombaini za wilaya Unguja, Pemba

Na Salum Vuai, Maelezo

KAMATI ya Central Taifa Zanzibar, imeandaa mashindano ya soka kuwania Kombe la Mapinduzi kwa timu za vijana walio chini ya miaka 20 kutoka wilaya kumi za Unguja na Pemba.

Michuano hiyo itakayoshirikisha pia timu ya taifa ya vijana walio chini ya miaka 17, imepewa jina la ‘Abeid Amani Karume Cup.


Katibu wa kamati hiyo Abdallah Thabit ‘Dula Sunday’, ameliambia gazeti hili kuwa, ngarambe hizo zimepangwa kuanza kutimua vumbi Januari 3 na kufikia tamati Januari 12, 2012.

Alifahamisha kuwa, kila wilaya itawakilishwa na kombaini yake katika hatua ya kwanza ya makundi, na baadae bingwa wa Pemba na yule wa Unguja, watacheza fainali kutafuta bingwa wa mashindano hayo yaliyoanzishwa kuongeza vuguvugu la sherehe za Mapinduzi matukufu ya Januari 1964.

Alivitaja viwanja vitakavyotumika kuendeshea michuano hiyo, ni Gombani na Kinyasini kwa upande wa Pemba, na kwa Unguja, mechi hizo zitarindima kwenye viwanja vya Mao Dzedong, Bungi, Mkwajuni,
Makunduchi na Mahonda.

Alisema fainali ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Januari 12, ambayo ni siku ya kilele cha sherehe za Mapinduzi, katika uwanja wa Amaan, wakati wa mchana, kabla ile ya mashindano mengine kama hayo iliyopangwa kuchezwa saa 2:00 usiku.

Alieleza kuwa, kamati yake iko katika mazungumzo na kampuni kadhaa kutafuta udhamini wa michuano hiyo, na kwamba yamefikia hatua nzuri ya kutia matumaini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.