Habari za Punde

ZANZIBAR MBIONI KUUNDA SHERIA KUKABILI RUSHWA

Na Mwantanga Ame

ZANZIBAR bado inafanya vizuri katika kukabiliana na rushwa ya kimataifa zinazotokana na mikataba ya zabuni za ujenzi zinazoingia serikalini.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheir, aliyasema hayo jana katika kituo cha televisheni cha ZBC, wakati akitoa taarifa maalum ya serikali juu ya kuadhimisha siku ya
kimataifa ya kupambana na rushwa.


Waziri huyo alisema ingawa bado kuna matatizo ya kuwepo viashiria vya matukio ya rushwa, lakini Zanzibar iko katika hali nzuri kupambana na rushwa katika mikataba ya kimataifa inayohusu zabuni za ujenzi.

Alisema hali hiyo inatokana na mikataba mingi ya kimatafa ilioyoingia serikali katika eneo la zabuni za ujenzi imekuwa ikifungwa na mashirika yanayotoa misaada ama mikopo na serikali hubakia katika eneo la kulipia gharama za ndani katika miradi inayokubaliwa.

Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo alisema serikali imekuwa inashindwa kuingilia utaratibu huo kwa vile ni sehemu ya masharti wanayopewa na taasisi hizo za kimataifa jambo linaloepusha vishawishi vya rushwa ya
moja kwa moja.

Alisema katika utaratibu huo, taasisi hizo ndizo zenye kusimamia tenda za kupatikana makandarasi, jambo linaloifanya serikali kuepukana na rushwa ya kimazingira na hata rushwa kubwa.

Alisema baadhi ya nchi huingia moja kwa moja kwenye rushwa na kusababisha matatizo mengi ikiwemo kusimamishiwa misaada ama uwajibika kupungua kutokana na kuwepo kwa mazingira ya rushwa.

Alisema katika kupambana na tatizo hilo kitaifa na kimataifa hivi sasa serikali inajiandaa kuanzisha mamlaka ya kuzuia vitendo vya rushwa mswada ambao unatarajiwa kufikishwa katika Baraza la Wawakilishi
katika kikao kijacho.

Alisema mswada huo baada ya kupitishwa na kuwa sheria kamili, serikali ya Zanzibar inatarajia itaweza kukabiliana na tatizo hilo kwa kiasi kikubwa .

Waziri huyo alisema kwa upande wa Zanzibar maeneo ambayo yanajengewa dhana ya kuwapo kwa mazigira ya rushwa kwa kiasi kikubwa serikalini ni yale yanayohusu sehemu za manunuzi ya vifaa na ugavi.

Hata hivyo, alisema inawezekana kuwepo maeneo mengine, lakini bado tathmini halisi ya tatizo la ruswa Zanzibar haijafanyika kwa vile inasimamia kupatikana mamlaka hiyo kwa haraka ili kuweza kujua ukubwa
wa tatizo hilo.

Alisema wakati serikali ikisubiri sheria hiyo ikamilike bado itaendeleza juhudi kuhakikisha rushwa inapungua ama kumalizika kabisa.

Jambo la msingi alisema wananchi watapaswa kushiriki kwa pamoja katika kufichua wala rushwa kwani mazingira ya sheria mpya yataweza kumpa haki ya ulinzi katika hatua za awali.

Alisema suala la kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada hizo ni muhimu kwa vile Zanzibar inalazimika kuingia katika mapambano hayo kwa vile Tanzania iliridhia mkataba wa kimataifa wa kupambana na rushwa
wa mwaka 2003.

Kutokana na ukweli huo, alisema Zanzibar imeamua kuadhimisha siku hiyo juzi baada ya tarehe rasmi ya dunia ya Disemba 9, kwa vile iliingiliwa na sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.

Waziri Haji alisema, Wizara hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa inaadhimisha siku hiyo inakusudia kufanya maonyesho mbali mbali yatayokuwa yakiizindua jamii na vitendo vya rushwa ikiwa pamoja na kufikisha
ujumbe wa mwaka huu unaosema ‘chukua hatua dhidi ya rushwa leo’

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.