Na Mwantanga Ame
RAIS Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, amesema kauli ya ‘mapinduzi daima’ isiwatishe wananchi, kwani maana yake halisi ni kuwapatia wananchi wa Zanzibar mageuzi ya kimaendeleo.
Dk. Karume, alieleza hayo jana wakati akifungua jengo jipya la skuli ya Mwembe Shauri, iliyojengwa kwa msaada ZAYADESA, kwa kushirikiana na serikali Mbunge, Mwakilishi na wadau wengine.
Alisema kwa muda mrefu wapo baadhi ya watu wamekuwa na wasiwasi juu ya kauli hiyo kwa dhana wanazozijua wao, ambapo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwani dhamira ya serikali ya juu ya kauli hiyo ni kuwapatia wananchi maendeleo daima.
Alisema serikali ya ukoloni haikuwapa fursa wananchi wote kupata nafasi ya kusoma kutokana na kuwapo kwa skuli chache na idadi ya wanaopata elimu ilikuwa ni ndogo, huku serikali hiyo haikuwa ikichukua
bidii kufanya mabadiliko yoyote katika sekta hiyo.
Alisema baada ya Mapinduzi 1964, serikali iliyoingia madarakani iliweza kuibadili sekta ya elimu kila mwaka kwa kutoa elimu bure, jambo ambalo limeongeza idadi ya skuli na kutoa nafasi zaidi kwa wananchi wa Zanzibar kupata elimu.
Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo Dk. Karume, alisema ndio maana serikali ya Zanzibar imekuwa ikisema mapinduzi daima kwa vile hayo ni maendeleo ambayo yamepatikana baada ya Mapinduzi kwani kabla ya hapo hayakuwapo.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inapenda kuona inawapatia wote fursa za kupata elimu na ndio maana imekuwa ikichukua juhudi kujenga majengo mapya na ya kisasa ili wananchi watumie fursa hiyo bila ya ubaguzi kama ilivyokua wakati wa ukoloni.
Alisema Zanzibar tangu kuanza kutekeleza sera ya maendeleo katika sekta ya Elimu, Zanzibar imekuwa nchi ya mfano ikilinganishwa na nchi nyengine katika bara la Afrika.
Alisema hiyo tangu kutangazwa kwa malengo ya Milenia zipo juhudi mbali mbai ambazo serikali imezichukua kuibadili sekta ya elimu kiasi ambacho tayari imeweza kuifikia dhamira hiyo.
Akizungumzia juu ya uhuru unaodaiwa kupatikana mwaka 1963, alisema hilo halipo kwani ulikuwa ni wa bandia na aliyepewa uhuru huo ulikuwa ni utawala wa kisultani.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Karume, alisema uhuru wa Zanzibar ni wa 1964, ambao ulitokana baada ya kuondolewa madarakani utawala wa mkoloni.
Alisema uhuru huo ndio ulitambuliwa na dunia nzima yakiwemo mataifa ya Afrika, huku nchi zilizokuwa zikiitawala Zanzibar ikiwemo Uingereza ndio iliyochelewa kuutambua uhuru huo.
Mapema Dk. Karume aliifungua rasmi jengo la skuli ya Mwembe Shauri ambapo katibu Mkuu wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh, akitoa maelezo ya kiufundi alisema thamani yake hadi
linakamilika ni shilingi milioni 222,492,444.
Alisema kati ya pesa hizo serikali ya Zanzibar imetowa shilingi milioni 122,813,524 na ZAYADESA imetoa shilingi 99,678,920 ikiwa ni mchango kwa ajili ya kununulia vifaa pamoja na kuwalipa mafundi.
Mapema Mwalimu Tatu Suleiman Ubwa, akisoma risala ya Walimu wa skuli hiyo waliishukuru Jumuiya ya ZAYADESA na serikali kwa kufanikisha ujenzi wa skuli hiyo na kuiomba kuangalia uwezekano wa kujenga skuli nyengine inayofanana na hiyo kwenye eneo hilo.
Katika sherehe hizo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZAYADESA, Mama Shadya Karume, Mbunge wa Jimbo la Rahaleo Abdalla Juma na Mwakilishi Nassor Salum ‘Aljazira’.
No comments:
Post a Comment