Habari za Punde

Small Tiger yaikwamisha Machomanne

Na Abdi Suleiman, Pemba

PAZIA la ligi daraja la pili taifa Pemba, limefungwa juzi katika uwanja wa Gombani, kwa timu ya Small Tiger kutoka Mkoani kuichapa Machomanne United magoli 3-0.

Katika mtanange huo wa kundi B uliokuwa wa kasi na kusisimua, ambapo kila timu ilitaka kujihakikishia kushika nafasi ya pili, Machomanne ilikuwa na kazi ngumu kwani ilihitaji ushindi wa mabao saba safi ili
iweze kushika nafasi hiyo.


Mabao yaliyozima ndoto za Machomanne, yalipachikwa nyavuni na Omar Zaidi katika dakika ya 15, Masoud Salum (dk 30), huku Mohammed Khamis akihitimisha ushindi huo kwa mkwaju wa penalti.

Kwa matokeo hayo, timu ya Small Tiger imefikisha pointi 20, huku ikisubiri mchezo wake dhidi ya Fufuni SC ulioshindwa kuchezwa Januari 16 baada ya waamuzi kutokufika katika uwanja wa Mjimbini.

Ligi hiyo imegaiwa katika makundi mawili, ambapo kundi A linaongozwa na timu ya Coast Boys yenye pointi 21 ikifuatiwa na African Kivumbi iliyokusanya pointi 19, wakati Fufuni SC yenye pointi 25 inaongoza kundi B, huku Okapi yenye pointi 21 ikisubiri hatima yake katika mchezo wa FSC na Small Tiger kujua timu itakayoshika nafasi ya pili.

Timu ya FSC na Coast Boys tayari zimeshakata tiketi ya kucheza ligi daraja la kwanza taifa Pemba msimu ujao, huku African Kivumbi ikisubiri kucheza na Small Tiger au Okapi ili kupata timu itakayoungana na FSC na Coast Boys, zote kutoka Wilaya ya Mkoani.

 Timu za Red Star ya Mkoani, Chuoni na Mchangamdogo United, zote zimeshindwa kuhimili vishindo vya ligi hiyo na tayari zimeshateremka hadi daraja la pili Wilaya ya Wete msimu ujao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.