Habari za Punde

Ireland, Zanzibar Kuendeleza Ushirikiano

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

IRELAND imeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar na kueleza kuvutiwa kwake na juhudi za maendeleo zinazochukuliwa kwa mashirikiano ya pamoja hapa nchini, chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Lorcan Fullam, aliyasema hayo alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,Ikulu mjini Zanzibar.

Balozi Fullam, ambaye amekuja kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini, alimueleza Dk. Shein kuwa Ireland inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kuahidi kuuimarisha zaidi.

Alisema kuwa Ireland inatambua juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano ya pamoja kati ya wananchi na viongozi wao katika kuimarisha sekta zake za maendeleo chini ya uongozi wa Dk. Shein.

Aidha, Balozi Fullam, alimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo ambazo nchi hiyo imeahidi kuendelea kuziunga mkono.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa shukurani kwa Balozi huyo na nchi yake ya Ireland kwa ushirikiano uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia magari ya zimamoto katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Alisema hatua hiyo imesaidia zaidi katika kutoa huduma za zimamoto uwanjani hapo na kusisitiza kuwa hivi sasa mahitajio yatazidi kuongezeka kutokana na juhudi za Serikali za upanuzi na ujenzi wa uwanja huo pamoja na ahadi kutoka kwa mashirika mbali mbali ya ndege yaliyoahidi kuleta ndege zao hapa Zanzibar likiwemo Shirika la Qatar Airways, Emirate, Arabian na mengineyo.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika hatua za kuendeleza na kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo hasa cha umwagiliaji maji kwa kutambua kuwa kilimo hicho ndio chenye tija kwa wakulima hivi sasa.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimuelezea Balozi Fullam mikakati ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini iliyowekwa na Serikali pamoja na juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanaimarika nchini.

Alisema kuwa mashirikiano ya pamoja yameweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha maendeleo huku wananchi wakiwa na matumaini makubwa juu ya serikali yao inayowaongoza kutokana na juhudi inazozichukua.

Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo ni changamoto kubwa kwa uongozi na wananchi kwa jumla kutokana na matarajio hayo ya wananchi, hivyo inampasa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa umoja, amani na utulivu uliopo nchini sanjari na mashirikiano makubwa ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi kwa jumla kutazidi kuiletea Zanzibar mafanikio na maendeleo makubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.