Habari za Punde

Jiji la Arusha latakiwa kuimarisha usafi

Mahmoud Ahmad, Arusha
JIJI la Arusha limetakiwa kuweka mkakati wa kukusanya kodi ya majengo, sambamba na kuboresha usafi ili kuvutia watalii wanaotembelea jiji hilo.

Mstahiki Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Dar-es-salaam, Songoro Mnyonge, akiwa pamoja na ujumbe wake walipotembelea jiji la Arusha, alisema wakati umefika sasa wa halmashauri ya jiji la Arusha kukuza zaidi ukusanyaji wa mapato kwa nia ya kuongeza mapato kwa Serikali.

Alisema mapato mengi yamekuwa yakipotea kutokana na upotevu mkubwa wa fedha kwa watendaji kuwaonea muhali wamiliki wa majumba hali inayofanya kukosa kodi za majengo na kuporomosha mapato ya halmashauri nyingi hapa nchini.

Akitoa mfano kwa halmashauri ya manispaa ya Kinondoni inapata kiasi cha shilingi bilioni 25 katika mapato ya ndani kwa wakazi milioni 1.5, ambapo halmashauri ya jiji la Arusha inakusanya shilingi milioni .9 kwa wakazi wapatao 500,000

Hata hivyo, Mnyonge alisema pamoja na kubadilishana uzoefu lakini pia wameweza kulifahamu jiji la Arusha na maeneo ya vivutio vya utalii wa jiji katika eneo la Meserani snake park, mlima suye, na machinjio ya Arusha Meat.

“Tumejifunza mambo mbalimbali kuhusiana na shughuli za kitalii hususan hili la machinjio hivyo naamini tutakaporudi na sisi tutaanzisha sehemu nzuri na salama ya machinjio kwa lengo la kuboresha manispaa yetu”, alisema.

Songoro alisema hapo awali halmashauri ya jiji la Dar es salaam ilikuwa na mpango wa kuanzisha machinjio ya kisasa kama haya lakini hayakufanikiwa, hivyo halmashauri ya kinondoni itachukuwa jukumu la kujenga machinjio hayo ilikuondokana na kuchinja wanyama kiholela.

Nae Kaimu Meya wa jiji la Arusha, diwani wa kata ya baraa, Paul Loti Laizer, alisema halmashauri Ya jiji la Arusha inakabiliwa na changamoto ya usafi.

Alisema tatizo hilo, wanakusudia kuliwekea mkakati ili liwe mfano kwa masoko mengine ili kujiepusha na magonjwa ya milipuko kwa watu kufanya biashara chini na njiani.

Laizer alisema kuwa wamejifunza mambo mengi kwenye ziara hizo na ni na watakaporudi wanaazimia kuwa halmashauri ya Kinondoni kuwa mabalozi wa kuutangaza utalii wa ndani.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.