Apata Ushindi wa Kishindo Asilimia 94
Na Salum Vuai, Maelezo
Na Salum Vuai, Maelezo
HATIMAYE Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimepata Rais mpya kufuatia mgombea
pekee wa nafasi hiyo Amani Ibrahim Makungu kushinda kwa kishindo katika
uchaguzi mdogo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Salama hoteli ya
Bwawani.
Makungu alimudu kuzoa kura 49, sawa na asilimia 94 ya kura zilizopigwa kutokana
na wajumbe 52 wa mkutano mkuu wa ZFA, ambapo ni kura tatu tu ndizo
zilizomkataa.
Katika uchaguzi huo ulioendeshwa chini ya usimamizi wa kamati ya uchaguzi ya
chama hicho iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Gulam Abdallah Rashid, wapiga kura
walipata fursa kumuuliza mgombea huyo masuala juu ya namna atakavyoendeleza
soka la Zanzibar iwapo atachaguliwa.
Akijibu masuala hayo, na baada ya kutangazwa kwa matokeo, Rais huyo mteule
alisema, kimsingi ana dhamira ya dhati kuleta mabadiliko katika soka la
Zanzibar kwa wilaya zote Unguja na Pemba ili kurejesha hadhi ya visiwa hivi
kisoka.
Aidha alisema anakusudia kutumia kila uwezo alionao, pamoja na kubuni njia
chanya za kutafuta fedha, ili ZFA iondokane na aibu ya kuwa ombaomba na hivyo
kuendesha vyema shuguli zake na kuwapa matumaini Wazanzibari.
"Pamoja na nia yangu safi katika kuleta maendeleo ya soka, ieleweke kwamba
hili si jambo la mtu mmoja, tutafanikiwa kwa ushirikiano wetu sote, hivyo
naomba wajumbe na viongozi wenzangu, tushirikiane katika hili", alieleza
Makungu.
Makungu pia, aliwashauri wajumbe hao waridhie pendekezo lake la kutaka kuajiri
mtu atakayekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ufundi na Utawala, ambaye atakuwa
analipwa na chama hicho, wazo ambalo wajumbe walilipokea ingawa walisema
linahitaji kujadiliwa katika mkutano mkuu kabla ya kutoa baraka.
Aliyekuwa Rais wa ZFA kabla kujuzulu Ali Ferej Tamim, alikaribishwa kuzungumza
baada ya uchaguzi huo, ambapo alisema anaamini mrithi wake huo ni kijana mwenye
uwezo wa kuifanya vyema kazi ya kuongoza soka hapa nchini.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwa amejiuzulu, na uzee wake, yuko tayari kumsaidia
Makungu na ZFA kwa jumla, kwa ushauri juu ya njia bora za kuliimarisha soka la
Zanzibar.
Nafasi ya urais wa ZFA ilikuwa wazi kwa miezi mitatu kuanzia Machi 2, mwaka huu
kufuatia aliyekuwa akiishikilia kwa zaidi ya miongo miwili Ali Ferej Tamim,
kujiuzulu kwa sababu za kiafya na kutingwa na majukumu ya kifamilia.
Hongera Amani, tunataraji utatekeleza majukumu na ahahi zako katika kuendeleza soka Zanzibar.
ReplyDelete