Habari za Punde

Serekali Imezuiya Utoaji wa Viwanja Matemwe.

SERIKALI ya Zanzibar imesema imezuiya utoaji wa viwanja kwa wananchi wa kijiji cha Matemwe baada ya kujitokeza migogoro kati ya wananchi na serikali.

Naibu Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Salim Abdalla Hamad, aliyetaka kujua ni kwanini utoaji wa viwanja hivyo umesita kufanyika.

Akijibu suala hilo , Naibu waziri huyo, alisema ni kweli zoezi hilo limesita kufanyika baada ya kujitokeza kwa mizozo ya Wananchi.

Alisema nia ya serikali kuona inatoa viwanja hivyo kwa wananchi lakini haiwezi kuifanya kazi hiyo wakati kukiwa kuna mazingira ya mzozo jambo ambalo litaweza kuleta matatizo kati ya jamii na serikali.

Akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Wanawake, Salma Mussa Bilal, alietaka kujua Wizara hiyo ina mpango gani kuimarisha miundo mbinu ya maji, umeme na barabara katika maeneo ambayo yamepimwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makaazi.

Akijibu suala hilo Naibu huyo alisema dhamira ya serikali ni kuona inawapatia huduma bora wananchi za makazi lakini kazi hiyo imekuwa ikiifanya kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa baada ya kupata misaada.

Alisema kutokana na kuwapo kwa uwezo mdogo wa serikali ni vyema kwa wananchi waliopewa maeneo hayo kushirikiana na serikali ili kuwepo upatikanaji wa huduma hizo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.