Habari za Punde

ZEC, wadau wajipanga kwa uchaguzi Bububu

Na Madina Issa
VYAMA vya siasa zinavyotarajia kuwapeleka wagombea wake katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu vimetakiwa kuteuwa wagombea wenye sifa na uwezo wa kuongoza ili waweze kuepukana na pingamizi zisizokuwa za lazima katika kipindi cha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu.

Msimamizi wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, Suluhu Ali Rashid alipokuwa akizungumza katika mkutano uliowashirikisha wadau wa uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuhusiana na uchaguzi wa jimbo hilo mkutano ambao umefanyika katika ukumbi wa EACROTANAL Mjini Unguja.

Alisema endapo wadau hao watakapoteua wagombea ambao watakuwa na sifa nzuri wataweza kufanikisha uchaguzi na kuufanya uwe bora na imara na bila ya kufanya upendeleo na mang’uniko ya aina yoyote.

Alisema wagombea watakaoteuliwa kugombea katika uchaguzi huo ni lazima wadhaminiwe kama ulivyoagizwa sheria zz uchaguzi kuwa adhaminiwe na chama chake ambao wanachama hao wasiopungua 25.

Alisema katika kufanikisha uchaguzi huo ZEC inawaomba viongozi wa vyama vya siasa ngazi za wilaya na wadau wote wa uchaguzi kushiriki kikamilifu na kuhakikisha kuwa amani na utulifu vinadumishwa.

Hata hivyo alifahamisha kuwa uchaguzi huo utatumia daftari la kudumu la wapiga kura lililotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na pia Tume itaweka hadharani daftari hilo ili watu wote wataoshiriki kwenye uchaguzi huo wajielewe.

Mapema akifungua mkutano huo Mjumbe wa Tume ya uchaguzi Mwanabaraka Maalim, alisema kuwa ni vyema kwa wadau watakaoshiriki katika uchaguzi huo kuondokana na majungu ili waweze kuufanya uchaguzi huo wende kwa haki na uwazi.

Hata hivyo wadau hao wametakiwa wawahimize wananchi kwenda kupiga kura na endapo wakishamaliza kupiga kura waondoke vituoni mwao kwa kugojea matokeo wakiwa majumbani mwao.

Aidha aliwafahamisha kuwa kila mdau ana haki ya kumpa mwenzake taarifa ya upigaji wa kura ili haki ya kila mtu aweze kutekeleza kwa kumchagua kiongozi aliyekuwa mzuri ili aweze kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Nao washiriki hao wameiomba ZEC kuweka ulinzi madhubuti ili kuweza kuendeleza amani iliyoko kwani kila kipindi cha uchaguzi huwa na vurugu.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.