Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Kilimo na Maliasili, Suleiman Othman Nyanga, amesema suala la utoaji wa ruzuku kwa wakulima wa Unguja na Pemba, linahitaji muda ili mafanikio yake yaweze kuonekana katika sekta ya kilimo nchini.
Waziri huyo aliyasema hayo jana alipokuwa akitoa ufafanuzi na kujibu baadhi ya hoja wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Waziri huyo alisema ruzuku za pembejeo za kilimo kwa wakulima ni miongoni mwa mambo yanayozisumbua nchi nyingi duniani, hivyo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji muda wa kujipanga ili kuweza kumudu utekelezaji wa mpango huo.
Alisema ingawa serikali ya Zanzibar imeamua kuanzisha utaratibu wa kuwapatia wakulima ruzuku ya pembejeo za kilimo, lakini bado imejikuta ikikabiliwa na changamto mbali mbali za kuendesha mpango huo.
Alisema katika mwaka wa fedha uliopita wizara hiyo iliwapatia wakulima jumla ya tani 322 za mbegu bora za mpunga kwa msimu huu wa mwaka 2012 ikilinganishwa na tani 124 ya mwaka 2011 na tani 55 za mwaka 2010.
Kwa upande wa mbolea na dawa ya kuulia magugu, waziri huyo alisema lita 20,000 za dawa hiyo ilinunuliwa ikilinganishwa na lita 18,000 kwa mwaka 2011 na tani 590 za mbolea aina ya TSP tani 245 na UREA tani 18 345 ikilinganishwa na tani 330 kwa mwaka 2011.
Akizungumzia juu ya kiwango cha mbegu zilizopatikana waziri huyo alisema ni jumla ya tani 322 za mbegu ya mpunga zikiwemo tani 21 za mbegu ya NERICA zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima.
Aidha, Waziri huyo alisema kwa wilaya ya Kaskazini ‘B’, juu ya suala hilo mbegu bora zilizotolewa kwa wakulima ni tani 113.8 mbolea ya UREA tani 28, TSP tani 30 na dawa za kuulia magugu lita 3,500.
Waziri huyo alisema mbolea ya ziada ambayo serikali ililazimika kuiingiza kutoka Tanzania Bara, waziri huyo, alisema ni tani 100 na sio tani 200 kama ilivyodaiwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo wakati wakitoa michango yao.
Hata hivyo Waziri huyo alisema mbegu hizo zilizoagizwa zilikuwa na viwango baada ya kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na hivi sasa tayari Wizara hiyo imezigawa kwa wakulima wa Unguja na Pemba.
Kuhusu suala la ununuzi wa mbegu kwa wakulima wanaojitolea kuotesha waziri huyo alisema serikali ilinunua mbegu hizo tani 162, na itaendelea kufanya hivyo kila inapoona ipo haja na wakulima wanapaswa kuendelea kuzalisha mbegu hizo.
Hata hivyo kiasi hicho cha pembejeo ambacho walipatiwa wakulima wa Unguja na Pemba, waziri huyo alisema ilionekana kuwa bado kuna mahitaji makubwa jambo ambalo lilichangia kutokea kwa baadhi ya matatizo kwa wakulima hao kutopata mahitaji hayo kwa uhakika.
Alisema katika msimu ujao wa kilimo, wizara hiyo inakusudia kuongeza matrekta mapya 20 na kununua mbolea ya UREA tani 1000, TPS tani 500, dawa ya magugu lita 30,000, na mbego bora ya mpunga tani 570 na kutumia daftari la wakulima kwa ajili ya ugawaji wa pembejeo hizo.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, akisaidia kujibu baadhi ya hoja alisema, serikali tayari iko kwenye hatua mbali mbali ya kuimarisha uzalishaji wa matunda ili kuwawezesha wajasiriamali wa Zanzibar kuweza kujiajiri katika sekta hiyo.
Alisema katika mkakati huo ambao serikali imeuandaa ni pamoja na kufikiria kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawezesha kutumiwa na wazalishaji wa matunda kuzalisha bidhaa zao.
Akijibu hoja ya Mwakilishi wa Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa, aliyetaka kujua utaratibu uliotumika wa kulitoa shamba la kilimo huko Micheweni, waziri Aboud, alisema suala hilo lilitolewa na Idara ya Ardhi na wizara hiyo italifuatilia na kuona vipi wanalifanyia kazi ili shamba hilo lirudi mikononi mwa wizara husika.
Kuhusu suala la tathimini ya vipando juu ya wakulima waliokuwa wakifanya shughuli zao Bungi ambapo umehamishiwa mnara wa matangazo ya redio, ambapo Waziri Aboud, alisema wizara mbili hizo zitakaa pamoja ili kulipatia suluhisho suala hilo.
Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 15.061 kwa mwaka wa fedha 2012/2013
No comments:
Post a Comment