Habari za Punde

Duni:Afya Zanzibar imepiga hatua kubwa

Na Salum Vuai, Maelezo
LICHA ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya Zanzibar, imeelezwa kuwa katika miaka mitano iliyopita ya kutekeleza mpango mkakati namba mbili mabadiliko makubwa yamepatikana.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana, ni pamoja na Wizara ya Afya kuimarisha rasilimali watu ambapo idadi kubwa ya wafanyakazi wake wamepatiwa mafunzo ya ngazi na taaluma mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Akifungua mkutano mkuu wa saba wa Wizara ya Afya unaofanya mapitio ya utekelezaji wa mipango yake kwa mwaka unaomalizika huko katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Waziri wa wizara hiyo Juma Duni Haji, alisema kwa sasa, kuna wanafunzi 1,435 wanaopata mafunzo, ambapo 188 kati yao wako nje ya nchi.

Duni alieleza kuwa, huduma za afya zimeimarika Unguja na Pemba, sio tu kwa kuweka mamlaka na dhamana katika ngazi za wilaya, bali pia ugawaji wa rasilimali za watu, vifaaa na fedha.

Aidha, alisema ufanisi mkubwa umepatikana katika kuimarisha huduma za afya ya mtoto na mama kutokana na mikakati mizuri na utumiani bora wa raslimali adimu zinazopatikana.

Waziri huyo pia alitaja mafanikio mengine, kuwa ni kwa makundi maalumu kuhakikishwa huduma bora na ziazopatikana kirahisi, akiyataja makundi hayo kuwa ni ya wanawake, watoto, watu watu wenye ulemavu na masikini wa kupindukia.

Alifahamisha kuwa, sekta ya afya katika kipindi ca miaka mitano iliyopita, imekuwa ikitegemea fedha kutoka vianzio mbalimbali, ikiwemo mchango wa serikali kupitia kodi ya mapato, pamoja na washirika wa kimaendeleo kutoka nje ya nchi.

Akitoa mchanganuo, Duni alisema sehemu kubwa ya fedha hizo, zilitolewa na washirika wa nje wa maendeleo, ambao walichangia kati ya asilimia 62 na 65 kwa miaka ya 2006/09, na asilimia 55 mwaka 2010 wakati michango y ndani ukiwemo wa serikali, ulikuwa asilimia 43, mwaka 2010.

Alisema mabadiliko mengine ni kuimarika kwa uwazi na uwajibikaji ambayo ndio kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu, pamoja na ushirikiano, ambapo matumizi ya fedha yanafanywa kwa umakini mkubwa na wadau kupata taarifa kupitia mikutano ya aina hiyo.

Akizungumzia hali ya malaria katika visiwa vya Zanzibar, Duni alisema dhamira ya dhati, mikakati endelevu na ushirikishwaji wa wanajamii, vimesaidia sana katika vita vya kupambana na ugonjwa huo.

Alisema jitihada za kutokomeza malaria ziliongezeka zaidi mwishoni mwa miaka ya tisini na mapema miaka ya elfu mbili, na kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Zanzibar , washirika wa maendeleo na wadau, imewezekana kupunguza mzigo wa maradhi hayo na pia kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa.

“Kwa jitihada hizi na ushirikiano tunaopata, tumeweza kupungua malaria hapa nchini kwa kiwango cha hadi asilimia 0.7, na sasa ugonjwa huo sio tena kati ya yale kumi yanayosababisha vifo”, alieleza.

Alieleza matarajio yake kuwa mkutano huo wa siku mbili utajikita katika kujadili kwa kina changamoto kadhaa zinazoikabili Zanzibar ikiwemo kuongezeka kwa maradhi yasiyoambukiza kwa nia ya kuyatafutia ufumbuzi.

Mapema, Mwakilishi wa UNESCO hapa Zanzibar Ruth Leano, alisema Shirika lake pamoja na wahisani wengine, wanaridhika na kuthamini juhudi za Serikali ya Zanzibar katika matumizi ya fedha za misaada zinazotolewa.

Aidha, alisema mafanikio yaliyopatikana katika maeneo tafauti ya huduma za afya, ni ushahidi wa dhamira ya serikali kuhakikisha inaimarisha hali na ustawi wa wananchi wake.

Mkutano huo wa siku mbili unashirikisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, wafanyakazi na waalikwa mbalimbali kutoka nchi washirika wa maendeleo.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.