Na Mwantanga Ame
WAKATI zoezi la kutoa maoni kwa ajili ya kupatikana kwa Katiba mpya likiendelea visiwani Zanzibar, baadhi ya wananchi wamependekeza suala la madaraka ya Kadhi na Mufti Mkuu kuingizwa katika Katiba mpya.
Wananchi hao walieleza hayo wakati wakitoa maoni yao katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Mwera Wilaya ya Kati Mjini Unguja.
Akitoa maoni hayo, Sabri Abdalla (50) Mkaazi wa eneo hilo ambaye ni Mstaafu, alisema imefikia wakati ndani ya Katiba mpya madaraka ya Mufti Mkuu na Kadhi, yawekwe kikatiba.
Alisema kuingizwa kwa viongozi hao katika mfumo wa Katiba mpya kutaweza kusaidia kuondoa mivutano iliyokuwa ikijitokeza hivi sasa juu ya madaraka yao kutodharauliwa.
Eneo jengine ambalo Mwananchi huyo alishauri kuona linabakia kama lilivyo linalohusu serikali kubakia kuwa haina dini na suala la uhifadhi wa haki za binadamu kubakia katika usawa mbele ya sheria.
Aidha, Mwananchi huyo akiendelea alipendekeza suala la ardhi libakie chini ya usimamizi wa serikali ili kuepuka kutekwa na wawekezaji, pamoja na suala la maadili ya viongozi liwekwe vizuri ili liwezeshe kuwawajibisha viongozi kikatiba ili kuimarisha mfumo wa madaraka.
Akiendelea na maoni yake hayo Sabri alisema sera ya kujitegemea bado inahitaji kubakia huku suala la usawa wa kijinsia na makundi maalum nalo linawekwa katika misingi ya katiba.
Eneo jengine amabalo Mwananchi huyo alilitaja li la madaraka ya Rais yawe ya Rais Mtendaji na mfumo wa viongozi wakuu wa serikali katika Muungano uwe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais awe Rais wa Zanzibar, kuwepo kwa Makamu wa Pili wa Tanzania na Waziri Mkuu.
Pia mwananchi huyo akiendelea alisema eneo jengine ambalo linahitaji kubakia kama lilivyo ndani ya Katiba mpya linahusu Muungano wa serikali mbili na Zanzibar ibakie kuwa na serikali yake pamoja na serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mwananchi mwengine Madiwa Kurungwe (58), alipendekeza kwa serikali kufikiria kurejesha kwa darasa la nane na Muungano kubakia wa serikali mbili, haki za binadamu kulindwa na hifadhi ya mazingira izingatiwe ndani ya Katiba.
Eneo jengine ambalo limeguswa na wananchi wengi linahusu mfumo wa muungano wa serikali mbili huku wengine wakitaka kuwepo kwa Muungano wa Mkataba.
Wananchi waliopendekeza kuwepo kwa muungano wa serikali mbili ni Ndejemi Sid Juma (50), Mtumwa Ali Juma (38), Mgeni Ame Mussa, Mkitu Suleiman Juma, Flora Joseph Mtingwa, Uledi Baraka, Juma Abdalla Shija, ambaye alitaka elimu ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne iwe elimu bure pamoja na utoaji wa heka uondolewe na badala yake watu wawe wanapewa mashamba.
Nae Riziki Hassan Mussa (50), alitaka suala la maendeleo liangaliwe kutokana na hivi sasa, bado kuna watoto wanaokaa chini wakiwa skuli jambo ambalo limekuwa likiwasumbua kufanya usafi kwa kila siku.
Wananchi waliopendekeza mfumo wa serikali tatu ni pamoja na Omar Mussa (55), aliyetaka uwepo wa serikali ya mkataba, sarafu ya Zanzibar, kiti cha umoja awa kimataifa.
Hata hivyo mwananchi huyo, alilalamikia kuharakishwa kuanza kwa mfumo huo wa kuchukua maoni kwani ulikuwa unahitaji kuwapa muda zaidi wananchi ili wajiandae kama ilivyofanyika nchini Kenya.
Othman Hassan alisema mfumo wa sasa serikali mbili za Muungano umekuwa ukiikosesha Zanzibar kujiunga na FIFA pia kuwepo kwa mgombea binafsi kutoka ngazi ya chini na Abrahamani S. Abrahaman alietaka kuangaliwa kwa walemavu.
Ni wazi kwamba watu hawana elimu ya katiba kwani mambo mengi waliyoyazungumza hayahusu katiba ya Muungano,Zanzibar ina katiba yake na mambo kama (arhdi, elimu ya msingi na kati, afya, michezo, usawa wa kijinsia) sio mambo ya Muungano bali yamo katika katiba ya Zanzibar. Hayo ni matokeo ya kuwaburuza watu kwa muda mrefu na akitokea wa kuwapa elimu ndio hayo tena wako mahabusu kwa kesi za kupangwa na watu fulani kutekeleza matakwa yao.
ReplyDelete