Na Asya Hassan
SERIKALI imesema itaendelea kuunga mkono
utekelezaji wa mradi wa Tasaf awamu ya tatu ili kuzikwamua kaya maskini na hali
ngumu ya kiuchumi inayozikabili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd aliyasema hayo wakati akizindua mradi wa awamu ya tatu wa
TASAF kwa kanda ya Zanzibar hafla iliofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort
Mazizini.
Alisema lengo la serikali ya
Zanzibar ni kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na hali ngumu ya umaskini na utegemezi.
Alisema katika miaka mitano ijayo
mpango huo utawafikia walengwa milioni 1.5 Tanzania Bara na Visiwani wanaoishi
katika mazingira hatarishi.
Hata hivyo, alisema ili malengo
hayo yafikiwe ushiriki wa wadau wote unahitajika.
Aidha alisema ni matarajio ya
serikali kuwa mpango huo utaimaisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa
makundi mbali mbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini walengwa
katika shehia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema Tasaf awamu ya tatu utabeba
changamoto zote ambazo zilitokea awamu ya mwanzo na ya pili na kuzifanyia
marekebisho ili zisiweze kutokea katika awamu ya tatu.
Alisema Tasaf imetenga fedha za
kutosha katika kuyajengea uwezo mifumo yote ili kuweza kufikia lengo
lililokusudiwa.
Nae Katibu Mkuu Ofis ya Makamu wa
Pili wa Rais, Dk. Khalid Mohammed alisema TASAF awamu pili kwa Unguja na Pemba ilitekeleza miradi
820 ambapo Unguja ilikua miradi 433 na Pemba miradi 387.
Alisema kuwa fedha zilizotumika
katika miradi hiyo ni shilingi bilioni 12 ambapo bilioni 1.3 zilitolewa na
wananchi wenyewe.
No comments:
Post a Comment