Habari za Punde

Wenye ulemavu waruhusiwa kuunda baraza lao la katiba



Na Fatuma Kitima,Dar es Salaam
TUME  ya Mabadiliko ya Katiba imewakubalia watu wenye ulemavu kuunda baraza lao la katiba ambalo litakuwa likipitia rasimu ya katiba ambayo itatolewa  na  tume hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana,  Mwenyekiti wa maandalizi wa kamati ya Umoja wa Wajasiriamali walemavu Mkoa wa Dar es Salaam (UWAWADA), David Nyendo alisema kukubali kwa tume hiyo ni neema kwa  wenye ulemavu kusimamia haki zao katika katiba mpya.

Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,  Jaji mstaafu, Joseph Warioba amekiri kuwa suala la watu wenye  ulemavu kuwa na baraza la katiba lilikuwa halipo katika mlolongo wa mabaraza yatakayoundwa.

Alisema kuanzia sasa wanajipanga na kuhamasisha  mabaraza ya watu wenye ulemavu kila wilaya ambao ndio muungozo wa kusimamia haki za watu wenye ulemavu katika katiba mpya.


Aidha alisema walemavu wamefarijika  kuwepo kwa baraza la watu wenye ulemavu katika kila wilaya kutokana  na tume kujua umuhimu wao kushiriki katika mchakato huo.

Hata hivyo, alisema ushiriki wao katika mabaraza hayo utasaidia kupata katiba ambayo itakayokuwa inatambua haki zao.

Naye  Mwenyekiti wa Umoja wa wajasiriamali Wenye Ulemavu Mkoa wa Dar es Salaam, Kidumke Mohamed alisema watu ambao watachaguliwa katika mabaraza hayo wawe makini kuangalia vitu ambavyo vinawahusu watu wenye ulemavu na kuvisimamia kuingizwa katika katiba mpya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.