Habari za Punde

Maoni ya Muwaza Kuhusu Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano

 
                                                                                            20/02/2013
Mwenyekiti
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
S.L.P 1681
Dar-Es-Salaam

YAH: MAONI YA JUMUIYA YA MUSTAKABAL WA ZANZIBAR (MUWAZA) JUU YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
[A] UTANGULIZI

Jumuiya ya Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA) ni Jumuiya ambayo inawakutanisha Wa-Zanzibari walioko kote Ulimwenguni bila kujai itikadi wa mirengo ya kisiasa kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu ya Zanzibar kwenye nyanja za kijamii, elimu, Afya, Utamaduni na kisiasa.
Jumuiya ya MUWAZA imeanzishwa miaka mitatu iliyopita katika jiji la London nchini Uingereza yenye madhumuni yaliyotajwa hapo juu
[B] MADHUMUNI
Madhumuni ya hasa ya kuleta waraka huu ni kwa ajili ya kuchangia maoni yetu kwa Tume iliyochaguliwa hivi karibuni kwa ajili ya kukusanya maoni kwa ajili ya kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jumuiya ya MUWAZA ilifanya kikao chake jijini London siku ya Jumamosi, tarehe 19/01/2013 na kuamuwa kushiriki katika zoezi hili la kutowa maoni na kupendekeza kuwa ilivyokuwa nchi yetu ya Zanzibar ina katiba yake ya mwaka 1984 ambayo imeainisha mambo mengi tena kwa ufasaha kabisa. Kwahivyo, tumeonelea maoni yetu yalenge kwenye suala la Muungano tu ndio unaotukutanisha kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika.

Kama tunavyojuwa kuwa tokea ulipoasisiwa Muungano huu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Zanzibar na Tangania mwaka 1964 hadi hii leo kumekuwa na matatizo mengi ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kitamaduni ambao siku zote Zanzibar ndio hudhoofika zaidi siku hadi siku na kuitononesha Tanzania Bara (Tanganyika).  Kutokana na hayo ili kuborasha Muungano uliopo uwe imara zaidi, MUWAZA imependekeza mambo yafuatayo:-
1.      Pawepo Serikali mbili zilizo huru yaani Serikali ya Watu wa Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ambazo zitakuwa na Mamlaka ya kujiamulia kitaifa na kimataifa bila ya kuingiliwa ambazo zitaweza kujiwakilisha katika Umoja wa Mataifa, Umoja wa Africa, Jumuiya ya Madola na Mashirika mengine ya kimataifa;
2.      Pawepo Serikali ndogo ya Jamhuri ya Muungano itakayofungwa chini ya mkataba maalum baina ya Serikali ya Watu wa Zanzibar na Tanganyika ambazo zitakaa na kuangalia na kukubaliana mambo ambayo watashirikiana katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupata ridhaa ya Wananchi wa pande mbili za Muungano
 
Jumuiya ya MUWAZA inataraji kuwa utayapokea maoni yetu na kuyafanyia kazi kwa moyo mkunjufu
Natanguliza shukurani
 
Mwenyekiti
Jumuiya ya MUWAZA
UK

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.