Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizindua mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Vuga Mkadini ndani ya Jimbo la Kitope.
Nyuma ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo.
Picha na Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kujitahidi katika kuhakikisha huduma za Maji safi na salama ndani ya Jimbo hilo zinapatikana ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma hiyo Wananchi wake.
Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua mradi wa huduma za maji safi na salama katika kijiji cha Vuga Mkadini kilichomo ndani ya jimbo la Kitope.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Maji ni miongoni mwa huduma muhimu inayopaswa kutumiwa na kila mwanaadamu, hivyo Uongozi huo utachukuwa juhudi ya ziada katika kuona kero za upatikanaji wa huduma hiyo inakuwa ndoto ndani ya jimbo hilo.
Aliwaeleza Wananchi hao wa Kijiji cha Vuga Mkadini kwamba utaratibu mwengine utaangaliwa katika mpango wa kujenga Tangi jengine katika eneo hilo ili lisaidie kukidhi mahitaji ya maji ambayo kwa hivi sasa yanaendelea kuwa ya mgao.
Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi hao kuzingatia maagizo ya Wahandisi katika matumizi ya mashine zinazotumika katika Tangi la Kisima kilichopo Kijijini hapo ili zidumu kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
Akitoa Taarifa ya uzinduzi wa Mradi wa maji safi na salama wa katika Kijiji hicho cha Vuga Mkadini Katibu wa Kamati ya maendeleo ya Kijiji hicho Ndugu Hamad Mwinyi Ramadhan alisema huduma za maji safi ilikuwa ni kilio cha muda mrefu katika kijiji chao.
Nd. Hamadi alisema juhudi za Viongozi wa Jimbo hilo kupitia Mbunge huyo katika harakati za ziada za kujituma zimesaidia kuleta maendeleo ya haraka ndani ya Jimbo hilo.
“ Ukweli juhudi unazoendelea nazo siku hadi siku, hasa kilio chetu cha ukosefu wa Pump ya kupandisha maji na Switch Control Box zimeleta faraja na kwa kweli tunajisikia raha isiyo kifani“. Alisema Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Vuga Mkadini Nd. Hamad.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Wananachi wa Kijiji hicho Diwani wa Wadi ya Fujoni Nd. Hamad Khamis Hamad amempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif kupitia uratibu wa Mke wake Mama Asha Suleiman Iddi kwa kusimamia vyema maendeleo ya Wananachi wa Jimbo hilo.
Diwani Hamad alisema Wananchi wa Jimbo hilo wamekuwa wakishuhudia usimamizi wa Mbunge Kimawazo na hata uwezeshaji unaoendelea kuleta faraja na neema kwa wananchi hao.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif tayari ameshauzindua mradi wa Maji safi na Salama wa Kijiji cha Kipandoni uliogharimu shilingi Milioni 2,300,000/-, Kisima cha Maji Mgambo kiligharimu shilingi Milioni 4,000,000/- na mradi wa Vuga Mkadini umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 6,900,000/-.
Miradi yote mitatu imegharimu zaidi ya shilingi Milioni Kumi na Tatu na Laki Mbili { 13,200,000/- }.
No comments:
Post a Comment