Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Uongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania { TAMSA } kwenye dhifa ya ufunguzi wa mkutano wa Chama hicho Mbezi Beach Jijini Dar es salaam.
Kulia yake ni Rais wa Chama hicho Bwana Biswalo Yango na kushoto yake ni Mjumbe wa Sekriteriet ya Chama hicho Dr.Silu Selesta Gagela.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiufunguwa Mkutano wa kwanza wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania TAMSA hapo Mbezi Beach Royal Skyline Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania Tamsa mara baada ya kuufungua Mkutano wao wa kwanza hapo Mbezi Beach Royal Skyline Jijini Dar es salaam.
Picha na Hassan Issa, OMPR
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Juhudi za Madaktari katika kuzingatia utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ya kila siku kupitia msingi wa maadili uliowekwa katika fani hiyo ndio njia pekee itakayoendelea kuleta faraja miongoni mwa Wagonjwa pamoja na Wananachi wakati wanapohitaji kupatiwa huduma za afya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika dhifa maalum ya uzinduzi wa Mkutano wa kwanza wa Chama cha wanafunzi Madaktari Tanzania { TAMSA } uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Motel Royal Skyline Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif alisema wananchi wamekuwa wakiwalalamikia baadhi ya Madaktari na watendaji wa sekta ya Afya kutokana na huduma wanazotoa ambazo wakati mwengine huambatana na jeuri na dharau jambo ambalo linakwenda kinyume na maadili yao.
Alisema imani ya wananchi ni vyema ikarejeshwa na baadhi ya watendaji wenye tabia hiyo kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa wakielewa kwamba jukumu walilolibeba ni kazi ya wito inayohitaji hekma, ustahamilivu na uvumilivu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wanachama wa Chama hicho cha Wanafunzi Madaktari Tanzania { TAMSA } kwa juhudi zao za kuanzisha Taasisi hiyo yenye lengo la kuunganisha nguvu za pamoja za Madaktari hao.
Aliwahahikishia Wanachama hao kwamba Serikali zote mbili zitahakikisha kuunga mkono jitihada zao katika kuwapatia msaada unaostahiki zikiwemo fursa za masomo ya Juu katika ngazi ya Madaktari Mabingwa.
Balozi Seif alieleza kwamba Sera za Serikali zote ni kuimarisha miundo mbinu itakayowezesha kuwepo kwa kituo cha Afya kila baada ya kilo mita Tano ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma za afya wanachi hasa katika maeneo ya Vijiji.
Aliwaasa wanachama hao kujiepusha na migomo kwa kisingizio cha kutumia haki yao ya kidemokrasia katika kushinikiza madai au malalamiko yao kitendo ambacho huleta bughdha kwa wagonjwa na wakati mwengine kutishia kuhatarisha maisha yao.
Alieleza kwamba Serikali imekuwa ikitumia nguvu na gharama kubwa katika kuwaandaa madaktari kwa lengo la wamalizapo mafunzo waweze kutoa huduma kwa Umma Kitaalamu na kwa ufanisi zaidi.
“ Moja kati ya jambo ambalo Serikali isingependelea kuliona linaonekana ni migomo ambayo kwa kweli huleta fadhaa na wakati mwengine kuhatarisha maisha miongoni mwa wananchi “ Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Rais wa Chama cha Wanafunzi Madaktari Tanzania { TAMSA } Bwana Biswalo Yango aliipongeza Serikali Kuu kwa juhudi zake za kuunga mkono makundi mbali mbali ya Jamii hapa Nchini kikiwemo chama chao.
Hata hivyo Bwana Yango alisema Sekta ya Afya bado inaendelea kukabiliwa na changamoto kadhaa ambazo alizieleza kwamba ana imani kuwa zinaweza kutatulika kwa kutumia njia ya ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo.
Uzinduzi wa Mkutano huo wa kwanza wa Chama cha Wanafunzi Madaktari Tanzania { TAMSA } ulijumuisha mada tatu ikiwemo Historia ya Tamsa tokea kuanzishwa kwake.
Washiriki wa Mkutano huo pia walipata fursa ya kushiriki zoezi maalum la ununuzi wa keki pamoja na T. Shirt lililoongozwa na mgeni rasmi Balozi Seif kwa lengo la kusaidia kutunisha mfuko wa Chama hicho.
Wanachama wa Chama hicho kilichoanzishwa karibu miaka mitano iliyopita wanatoka katika vyuo Vikuu vya Afya Moi Muhimbili, Kairuki pamoja na International Medical Technology.
complement to TAMSA president and Honorable Second vice president of Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ReplyDelete