Habari za Punde

Ikulu Yasikitishwa na Gazeti Kumzulia Rais.

Na Mwandishi Wetu.
OFISI ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeelezea kusikitishwa na habari iliyochapishwa na gazeti la Nipashe toleo namba 057807 la Jumanne Julai 9, 2013 yenye kichwa cha habari “Shein amtolea Karume uvivu”

Katika habari hiyo imeelezwa kuwa kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti, mjini Unguja siku ya Jumapili tarehe 7 Julai, imeelekea kumlenga mtangulizi wake katika Ikulu ya Zanzibar jambo ambalo sio kweli.

Taarifa hiyo imesema kamwe maelezo ya Rais katika mkutano huo hayakumtaja mtu yeyote.

Taarifa hiyo imesema wajumbe wa Kamati ya Maridhiano wakiongozwa na kiongozi wao (siyo Dk. Karume) waliomba kuonana na Rais mara tatu, kupitia kwa Katibu wake, ambapo katika moja ya mikutano yao walimuomba awaunge mkono katika harakati zao za kutaka muungano wa mkataba.

Imeongeza Rais alikutana na Kamati ya maridhiano nyumbani kwake lakini hata mara moja hajawahi kukutana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Karume kwa mazungumzo nje ya ofisi yake ikulu.

Taarifa hiyo imesema katika mkutano huo Rais alieleza bayana kuwa alikutana na kiongozi wa kamati hiyo na wajumbe wake sasa inakuwaje ahusishwe Rais mstaafu Karume wakati yeye si kiongozi wa kamati hiyo?

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa Dk. Shein hana tatizo la watu au Wazanzibari kuwa na maoni yanayotofautiana lakini alichokikataa ni kuhusishwa yeye kuwa amebariki maoni ya kamati hiyo jambo ambalo siyo la kweli.

Ofisi hiyo imeelezea kusisitiza kuwa inaheshimu uhuru wa kuandika habari na pia kuheshimu wanataaluma katika sekta ya habari lakini imesikitishwa kuona mwandishi wa gazeti hilo ameamua kwa makusudi kuupotosha umma kwa kulazimisha maoni yake na kuyafanya kuwa kauli ya Rais.

Imeongeza kuwa kauli ya Rais katika mkutano huo ilikuwa kauli thabiti ambayo ilieleweka kwa kila mwananchi aliyehudhuria mkutano huo na aliyesikiliza kupitia vyombo vya habari na kwamba haikulenga wala kuelekea kumlenga Rais mstaafu Karume.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.