Habari za Punde

Jela miaka 30 kwa kubaka


Na Shemsia Khamis, Pemba
MAHAKAMA ya Mkoa Chake Chake imemuhukumu kijana Ali Mohamed Ali (22) mkaazi wa Kwale Miburani, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kubaka.

Mshitakiwa alipatikana akimbaka msichana mwenye umri wa miaka 12 (jina linahifadhiwa).

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu wa mahakama hiyo, Khamis Ramadhan Abdalla.

Mbali ya kifungo, mshitakiwa alitakiwa kulipa fidia ya shilingi 200,000 kutokana na madhara aliyomsababishia msichana huyo.

Hakimu Ramadhan alisema ametoa adhabu hiyo baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo na shaka, mashtaka dhidi ya mshitakiwa huyo.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita, akiwemo muathirika wa tukio hilo na daktari.

Upande mashtaka alidai, kuna kumbukumbu nyingi zinazomuhusisha mshitakiwa na makosa ya ubakaji, hivyo akaiomba mahakama itoe adhabu kali huku mshitakiwa akidai ni kosa lake la kwanza.

Mwendesha mashtaka Ali Bilal alidai Januari 5 mwaka 2011 majira ya saa 6:30 mchana, huko Miburani Kwali Wilaya ya Chake Chake, mshitakiwa alimbaka msichana huyo na kumsababishia maumivu makali.

Wakati huo huo, mahakama kuu Zanzibar kanda ya Pemba, chini ya Jaji Mkuu Omar Othman Makungu imemuachia huru kijana Hamad Ramadhan Othman (27), aliehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mzee mwenye umri wa miaka 60.

Mshitakiwa huyo akikata rufaa kupinga adhabu hiyo, iliyotolewa na mahakama ya mkoa.

Akitoa hukumu ya rufaa hiyo, Jaji Makungu alisema ushahidi uliowasilishwa hauwezi kumtia hatiani mrufaani, kwa vile hata wakati wa tendo lilipotokea lilikuwa lina utata mkubwa kwani baadhi ya mashahidi walikuwa wakitaja nyakati tafauti.

“Ushahidi uliotolewa ni dhaifu mno, hivyo hauwezi kumtia mrufaani hatiani na kuanzia sasa mahakama imekuachia huru, ili uweze kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli nyengine za maendeleo,” alisema Jaji Makungu.

Baada ya mrufaani huyo kuachiwa huru, Jaji Makungu alimuamuru kurudi nyumbani na mrufaani aliinua mikono juu kumshukuru Mwenyezu Mungu na kumuombea dua Jaji huyo kwa kumuachia huru.

Licha ya kuachiwa huru, mrufani huyo tayari alikuwa ametumikia kifungo cha miaka mitatu.

Awali mrufaani huyo alituhumiwa kutenda kosa hilo Oktoba 3 mwaka 2008 majira ya saa 11.00 asubuhi huko Matale Wilaya ya Chake Chake ambapo ilidaiwa alimbaka mzee mwenye umri wa miaka 60 na kumsababishia maumivu makali.

2 comments:

  1. huyo jaji alomfunga huyo kijana mwenyewe hana akili, nchi gani duniani iliyokuwa na sharia ya kumfunga mtu miaka 30 kwa ubakaji?

    ReplyDelete
  2. kama ikiwa kweli kabaka hata akifungwa maisha ni sawa tu, kwa nini abake?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.