Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Bima Zanzibar Tawi la Lumbumba Jiijini Dar es salaa alipofanya ziara ya kuzitembelea Taasisi za SMZ zilizopo Dar.
Meneja wa Benki ya watu wa Zanzibar { PBZ } Tawi la Kariakoo Jijijni Dar es salaam Badru Idd akitoa maelezo ya utendaji wa tawi hilo na Lile ya Benki ya Kiislamu liliopo Lumumba mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyekuwa katika ziara maalum ya kutembelea Taasisi za SMZ zilizopo Jijini Dar.
Pembeni yao kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Makao Makuu Zanzibar Juma Amour Mohammed
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar wa Matawi ya Kariakoo na Lumbumba kwenye ukumbi wa Tawi la Benki hiyo inayotoa huduma za Kiislamu uliopo Lumumba Jijini Dar es salaam.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Uongozi pamoja na Wafanyakazi wa Shirika ya Bima la Zanzibar { ZIC } na ule wa Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } ndizo zilizopelekea kuongezeka zaidi kwa idadi ya wananchi na wateja wanaohitaji kupata huduma katika Taasisi hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuzitembelea ofisi za Taasisi hizo zinazotoa huduma katika Jiji la Dar es salaam na kuelezea kuridhika kwake na utendaji bora wa kisasa uliofikiwa na mashirika hayo.
Balozi Seif alisema licha ya kuvutiwa sana na utaratibu wao wa makusanyo ya mapato na matumizi ya wastani lakini bado watendaji wa taasisi hizo wanapaswa kujituma zaidi katika mbinu za kutafuta wateja kwa lengo la kwenda sambamba na ushindani uliopo wa kibiashara.
Alifahamisha kwamba mbinu za kumchunga mteja wakati wote zitafanikiwa endapo juhudi za ziada za utoaji huduma kwa mwendo wa kasi kupitia watendaji hao zitachukuliwa.
“ Tuna kila sababu ya kuyapongeza mashirika yetu haya kutokana na huduma zao zinazokwenda kwa kasi. Haya ni miongoni mwa mashirika yanayoinawisha uso Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tuna haki ya kujivunia “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Taasisi hizo za Bima na PBZ mbali ya kuendelea kujitangaza lakini pia kufikiria kuongeza matawi mengine zaidi katika maeneo yenye mkusanyiko wa wananchi wengi yakiwemo yale ya Vijijini ili huduma zao ziwe za uwiano katika maeneo yote ya hapa Nchini.
Alieleza katika kuzipa nguvu zaidi taasisi hizo Serikali Kuu itaangalia utaratibu wa kuzikatia Bima mali zake yakiwemo majengo mapya ya Ofisi za Serikali zinazoendelea kujengwa katika maeneo tofauti Nchini.
“ Hata nyumba zangu niko tayari kuzikatia bima, kinachohitajika kwa sasa ni nyinyi watendaji kunishawishi hadi nifikie kiwango cha kutekeleza wazo hilo muhimu “. Alieleza Balozi Seif.
“ Tumekuwa pia tukishuhudia mikopo mikubwa inayotolewa na Benki ya Watu wa Zanzibar na ii ni vyema ikaenda samba mba na uwekaji wa bima ya maisha ili kunusuru kiwango kikubwa cha mikopo kinachotolewa endapo mkopaji mwenyezi Muungu atamuhitaji “. Aliendelea kufafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa Taarifa ya Shirika la Bima Zanzibar na Utekelezaji wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Abdulnaasir Abdulrahman alisema hali ya soko inaendelea kuwa ya ushindani ambapo biashara kubwa ikitawaliwa na ile ya kinga za magari.
Alisema biashara hiyo inachangia zaidi ya asilimia 80% ya biashara yote hali inayopelekea uongozi wa shirika kufanya juhudi za kuandikisha biashara nyengine ambazo zina faida kubwa ikilinganisha na ya magari.
Mkurugenzi huyo wa shirika la Bima alifahamisha kwamba shirika hilo limeweza kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kutoka katika vianzio vyake mbali mbali sawa na asilimia 86% ya lengo lake ambalo ni kukusanya shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka 2013.
Abdulnaasir alisema Kanda ya Pwani Dar es salaam ni tegemeo kubwa la shirika kwa makusanyo yake ambapo katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu Ofisi hiyo tayari imeshakusanya shilingi Bilioni 2.1 ikiwa ni sawa na asilimia 87% ya makadirio ya mwaka.
Alisema katika kukabiliana na ushindani wa kibiashara shirika lake licha ya kufanya kazi zake Zanzibar lakini pia limeweza kujitanua kwa kufungua ofisi zaidi katika kanda za Pwani- Dar es salaam, Arusha, Mwanza, mbeya, Dodoma na Mtwara.
Naye akitoa Taarifa ya maendeleo ya Matawi ya Benki ya Watu wa Zanzibar yaliyopo Kariakoo na Lumumba Mjini Dar es salaam Meneja wa Tawi la Kariakoo Badru Idd alisema PBZ ilipanga kuwafuata wateja wake waliopo na wanaokwenda Tanzania Bara kikazi, kibiashara, kimasomo na wanaopita ambao wanahitaji huduma za Kibenki.
Meneja Badru alisema pamoja na kuwepo kwa ushindani mkubwa wa kibiashara lakini matawi hayo yameweza kufungua hesabu za wateja mbali mbali na kufikia elfu 8,360 kutoka 3,209 ikiwa ni ongezeko la asilimia 160% .
Alifahamisha kwamba amana za wateja zimekuwa kwa kiwango kizuri na kufikia Shilingi Bilioni 24.58 mwezi agosti mwaka 2013 wakati disemba 31 mwaka 2011 zilikuwa Shilingi Bilioni 3.99 ikiwa ni ongezeko la asilimi 516%.
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana na Uongozi wa shirika la Meli na Uwakala Zanzibar Tawi la Dar es salaam na kuwaasa kwamba wana kazi kubwa ya kulihudumia shirika hilo katika mazingira ya uwajibikaji.
Balozi Seif alisema shirika hilo linaweza kupoteza imani ya wateja kwa kufikia hatua ya kukata tamaa endapo uendeshaji wa taasisi hiyo hautakuwa wa kiwango na uhakika.
Shirika la Meli na uwakala limeasisiwa mwaka 1978 likiwa na Meli sita zikiwemo mbili zilizorithiwa kutoka ukoloni ambazo zilikuwa zikitoa huduma katika mwambao wa Afrika ya mashariki kuanzia Mtwara Tanzania, Zanzibar, Tanga hadi Mombasa Nchini Kenya.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } ambapo aliushauri uongozi wa shirika hilo kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuwapatia bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara kwa bei nafuu.
Balozi Seif alisema utaratibu huo unaweza kutoa fursa zaidi ya kuongeza kipato cha wafanyabiashara hao ambao wengi hawana uwezo wa kufuatilia bidhaa hizo katika maeneo mbali mbali ya mIkoa ya Tanzania Bara.
Akitoa Taarifa fupi Naibu Mkurugenzi muendeshaji wa shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } Suleiman Juma Jongo alisema lisha ya shirika hilo lililoasisiwa katika miaka ya 70 kuendesha shughuli za ununuzi na uuzaji wa karafuu lakini bado lina fursa ya kuendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
No comments:
Post a Comment