TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Shirika la Utangazaji Zanzibar- ZBC limepewa changamoto ya kutumia hazina kubwa ya uzoefu wa muda mrefu wa watumishi wake kujiimarisha na kuendelea kuwa shirika lenye uwezo na kukidhi matarajio ya Taifa.
Changamoto hiyo imetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akihitimisha Kikao cha Kujadili Ripoti ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa mwaka 2012/2013 na Robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2013/2014.
Afafanua kuwa ni kweli shirika hilo ni jipya lakini inayo hazina kubwa ya watumishi wenye uzoefu wa muda mrefu hivyo halina budi kutumia hazina hiyo kujiimarisha.
“Ni dhahiri kuwa Shirika ni jipya hivyo linahitaji kuwa na mtazamo mpya, mfumo mpya wa utendaji, mbinu mpya na vifaa vipya lakini hata hivyo linajivunia hazina ya watumishi wenye uzoefu wa muda mrefu hivyo” alieleza Dk. Shein.
Alibainisha kuwa agizo la Serikali kuanzisha shirika hilo lilikuwa na dhamira ya kukifanya chombo hicho kuendelea kuwa madhubuti zaidi kinachokidhi sio tu mahitaji ya Taifa lakini pia mahitaji ya jamii nzima ya wasikilizaji na watazamaji wake.
Kwa hiyo alieleza watumishi wake hawana budi kuunga mkono uamuzi huo wa Serikali kwa kuonyesha ari na kuu
taka uongozi wa shirika kuwapa watumishi vijana changamoto kufanya vizuri kuimarisha shirika ikiwemo kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara kuongeza ujuzi wao.
Kuhusu hoteli ya Bwawani Mheshimiwa Rais aliitaka menejimenti ya hoteli hiyo kongwe nchini kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya biashara ili iweze kukabiliana na ushindani.
“Menejimenti ni lazima ijielekeze kufanya shughuli zake kibiashara na kwa kuzitumia vyema huduma zilizomo katika hoteli hiyo na kufanya ubunifu katika kuvutia biashara” Dk. Shein alieleza.
Alibainisha kuwa pamoja na Serikali kuwa na mpango mbadala wa muda mrefu wa hoteli hiyo lakini uongozi unapaswa kutumia mapato inayoingiza kufanyia matengenezo hoteli hiyo na kuendelea kuwa katika hali nzuri kibiashara.
Katika maelezo yake hayo kwa Wizara Dk. Shein arejea wito wake wa kuzitaka Wizara kuainisha maeneo ya kipumbele ya utafiti ili Wizara ziweze kuwaelekeza watafiti katika maeneo hayo.
Awali akitoa taarifa katika kikao hicho Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alieleza kuwa moja ya changamoto inayoikabili Wizara yake ni kuhakikisha matangazo ya ZBC yanapatikana kikamilifu kisiwani Pemba.
Alibainisha kuwa hivi sasa “Kampuni ya Zanzibar Multiplex inakamilisha usambazaji wa matangazo hayo kwa kuunganisha mashine ya kurushia mawimbi ya matangazo iliyoko Nungwi Unguja na ile ya Mizemitumbi Pemba”
Aliongeza kuwa kazi ya uhamishaji wa vifaa vya dijitali kutoka mnara wa Zantel Konde Chanjaani kwenda mnara wa TTCL kwa ajili yakuimarisha matangazo katika mkoa wa Kaskazini Pemba imeshakamilika.
Kuhusu ukusanyaji mapato Waziri alieleza Wizara yake katika mwaka wa fedha 2012/2013 iliweza kuwasilisha katika mfuko wa Serikali jumla ya Tshs 3.2 bilioni sawa na asilimia 93 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 3.5. Kwa mwaka huu wa fedha wizara imepangiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 3.6.
No comments:
Post a Comment