Habari za Punde

Tahadhari ya Hali ya Hewa Iliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya hali ya Hewa Tanzania, (TMA), imetowa tahadhari kwa wananchi kuacha kuyatumia maeneo ya ukanda wa pwani, huku Watanzania wakiungana na na wenzao duniani kusherekea sikukuu za krismasi.

Mamlaka hiyo imeeleza ni juu ya wananchi kuchukua tahadhari hiyo, baada ya kubaini kuwepo kila ishara zinazoonesha kuwa kutakuwa na upepo mkali utaojitokeza ndani ya siku mbili zijazo.

Mkurugenzi Mkuu  wa Mamlaka hiyo, Dk. Agnes Kijazi aliyasema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana nchini kote.

 Alisema vipimo vya hali ya hewa vimeonesha uwezekano wa kujitokeza kwa uwepo wa upepo mkali, ambao unatarajiwa kusababisha mawimbi makali ya baharini.

Alisema upepo huo unatarajiwa kuvuma katika ukanda wa bahari ukiwa mkali kufikia kilomita 40, kwa saa, pamoja na mawimbi makubwa kuzidi mita 2 katika ukanda wote wa pwani, hali ambayo inaweza kuleta madhara kwa wakaazi wa maeneo hayo.

Alisema hali hiyo, inatarajiwa kutokea kutokana na kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hali ya hewa katika bahari ya hindi, karibu na visiwa vya Comoro.

Alisema upepo huo unatarajia kuwa na mvuto kutokea pwani ya nchini Somalia na kuna uhakika wa asilimia 60, kutokea kwa hali hiyo.


Maeneo ambayo aliyataja kuwepo kwa uwezekano wa kukumbwa na hali hiyo, Mkurugenzi huyo alisema ni pamoja na Mikoa ya Tanga, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na visiwa vya Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Mamlaka hiyo, imewataka wananchi kujiandaa na majanga hayo, hasa wananchi wanapenda kutumia fukwe kwa ajili wa mapumziko wakati wa sikukuu na mapumziko ya krismasi.

Alisema tahadhari zitakazochukuliwa na wananchi hao zitasadia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Leo waumini wa dini ya kikristo, wanatarajiwa kuanza rasmi kuadhimisha skukuu ya krismasi ikiwa ni uzawa wa kiongozi wa dini hiyo Yesu Kristo aliyezaliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita.Wengi wa watanzania katika Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine hupendelea kutumia fukwe ya Coco beach, na baadhi ya hoteli za kitalii, ambapo husherehekea kwa kuogelea baharini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.