Habari za Punde

Uturuki yaangalia uwezekano wa kufungua Ofisi ndogo ya Ubalozi Zanzibar

 Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uturuki Bwana Ahmet Davutoglu akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Uturuki ulioongozwa na Waziri wa Kigeni wa Nchi hiyo Bwana Ahmet Davutoglu.

 
 
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki Bwana Ahmet Davutoglu, Mshauri wa Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Kigeni wa Uturuki Bwana Ali Sarikaya.

Kushoto ya Balozi Seif ni Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania Bwana Ali Davotoglu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikuliu na Utawala Bora Dr. Mwinyihaji Makame Mwadini.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 
Na Othman Khalism Ame OMPR
 
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uturuki Bwana Ahmet Davutoglu amesema upo umuhimu mkubwa wa kuangalia upya uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Uturuki na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika njia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande hizo mbili.
 
Alisema Uturuki na Tanzania hasa Zanzibar zimekuwa na uhusiano wa karibu tokea mwanzoni mwa karne ya 16 wakati mataifa haya bado yakiwa katika himaya ya utawala wa Mataifa makubwa ya ulaya.
 
Bwana Ahmet Davutoglu alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
 
Alisema Serikali ya Uturuki inaangalia mazingira ya kutaka kufungua Ofisi ndogo ya Ubalozi wake Zanzibar mpango utakaokwenda sambamba na jitihada za Serikali hiyo kuyashawishi mashirika na makampuni ya usafiri kuanzisha safari za ndege na meli moja kwa moja kati ya Uturuki na Zanzibar.

 
Waziri huyo wa Mambo ya nchi za nje wa Uturuki alifahamisha kwamba mazingira hayo yana lengo la kuimarisha sekta ya utalii kwa kutoa fursa zaidi kwa Wananchi wa waturuki kuanzisha tena safari za matembezi kati ya pande hizo mbili.
 
“ Watalii wengi wa Uturuki hupendelea kutembelea nchi mbali mbali Duniani kwa kutumia zaidi usafiri wa Meli. Fursa hii tunaiangalia namna inavyoweza kutumiwa na watalii hao kwa kuandaliwa meli maalum itakayowasafirisha kati ya Uturuki na Zanzibar kwa kupitia Mombasa “. Alisema Bwana Ahmet Davutoglu.
 
“ Hata usafiri wa moja kwa moja wa anga kwa kutumia ndege maalum pia unahitajika kutumika ili kuwapa fursa zaidi watalii hao wa Uturuki kuchagua usafiri wapendao ili kuitembelea Zanzibar ”. Alifafanua Bwana Ahmet Davutoglu.
 
Akizungumzia Sekta ya Afya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki alieleza kwamba suala la Taaluma ya afya litaendelea kupewa msukumo kwa kutoa upendeleo maalum kwa Zanzibar ambayo badi inahitaji wataalamu zaidi wa fani hiyo ili kukidhi mahitaji yake.
 
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Sekta ya Utalii hivi sasa imepewa nafasi  ya juu katika mipango ya Kiuchumi na Maendeleo katika Mataifa mbali mbali Ulimwenguni.
 
Balozi Seif alisema Vijana wengi Duniani wanaendelea kufaidika na sekta hii kwa kuendesha maisha yao ya kila siku ambapo imesaidia  kuwapunguzia ukali wa maisha pamoja na kujiongezea kipato.
 
“ Tumeshuhudia Visiwa mbali mbali Duniani vilivyoimarisha miundo mbinu katika eneo la Utalii sasa vimeanza kufadika na Sekta ya Utalii inayoonekana kuchukuwa nafasi ya kwanza kiuchumi ulimwenguni “. Alisema Balozi Seif.
 
Akizungumzia suala la Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Uturuki kwa jitihada zake za kusaidia sekta ya afya Nchini Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
 
Alisema wananchi wamekuwa wakifaidika na huduma zinazotolewa na Madaktari mabingwa wazalendo waliopata taaluma yao Uturuki sambamba na huduma zinazotolewa na madaktari wa kujitolea wa Nchi hiyo wanaokuja kupiga kambi katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar kwa kutoa huduma za afya bila ya malipo.
 
Akigusia sekta ya kilimo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba Serikali ya Uturuki kupitia Ujumbe huo kuangalia uwezekano wa kusaidia taaluma ya kilimo cha umwagiliaji maji hapa Zanzibar.
 
Balozi Seif alisema Uturuki kwa vile ina wataalamu wengi wa fani hiyo inaweza kuunga mkono nguvu za wakulima wa Zanzibar katika mpango wa kuwaongezea kipato kupitia uzalishaji wa kitaalamu.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.