Habari za Punde

Balozi Seif Ali. Atoa Mchango Wake kwa Timu za Jimbo lake Kujianda Ligi za Mabingwa wa Wilaya Unguja 12.Bora.

 Nahodha wa Timu ya soka ya African Coast ya Upenja akipoke mkwanja wa shilingi 1,000,000/- kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif ili ziwasaidie kujianda kwa ligi daraja la Pili kanda ya Unguja 12 bora.
Wachezaji wa Soka wa Timu ya African Coast ya Upenja waliopanda dfaraja la Pili wakifuatilia hafla ya kupongezwa kwao na Mbunge wa Jimbo la Kitope kwenye ukumbi wa CCM Jimbo hilo hapo Kinduni.

Wachezaji wa Timu ya Kinduni City wakisikiliza nasaha za Mbunge wao wa Jimbo la Kitope Balozi Seif hayupo pichani wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza baada ya kupanda daraja la pili.

Na Othman Khamis OMPR.
Wakati huo huo Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alizipongeza Timu za Soka za African Coast ya Upenja na Kinduni City zilizomo ndani ya Jimbo hilo kwa kupanda daraja la Pili zikijiandaa kucheza mashindano ya 12 bora za Wilaya za Unguja.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mchango wa shilingi Milioni moja kwa kila timu pamoja na Mchele na mafuta vitakavyozisaidia timu hizo kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo muhimu.


Hafla hiyo fupi ilifanyika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “ B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aliwataka wachezaji wa timu hizo wajitahidi kupeleka ushindi ndani ya jimbo hilo, na hilo litafanikiwa iwapo watajikita zaidi katika kuimarisha nidhamu itakayowajengea sifa jimboni na Wilayani kwa jumla.

“ Jiepusheni na tabia ya kubishana na waamuzi kwenye mashindano yenu. Nakuombeni mtunze nidhamu michezoni mkielewa kwamba uwamuzi wa marefa ni kitu cha mwisho mnachopaswa kukizingatia “. Alisisitiza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba mbali ya mashindano lakini michezo wakati wote inajenga urafiki na kuondosha uhasama miongoni mwa wachezaji pamoja na Viongozi wanaosimamia mchezo huo.

Aliwakumbusha wachezaji hao wa soka kuimarisha  juhudi za mchezo huo ambao tayari umeshatoa fursa pamoja na nafasi pana katika eneo kubwa  la ajira hasa kwa vijana.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanasoka pamoja na viongozi hao wa Jimbo hilo Diwani wa Wadi ya Mgambo Bibi Pili Moh’d Said alimpongeza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif kwa juhudi zake anazochukuwa katika kuimarisha sekta ya Michezo Jimboni humo.

Diwani Pili alimuahidi Mbunge huyo kwamba misaada aliyoitoa kwa wachezaji wa timu hizo itatumika kwa lengo lililokusudiwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.