Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Mashina ya CCM Wilaya ya Magharibi Unguja.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Tifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi na Wanachama wa Shina la CCM Sharifu Msa akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa chama hicho ndani ya Mkoa wa Magharibi Wilaya ya Mfenesini Kichama. 

Balozi Seif akizungumza na Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mfenesini hapo Ofisi ya CCM Wilaya hiyo Mtoni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mfenesini wakifuatilia hotuba ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama.
 Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema nguvu za Chama cha Mapinduzi zitazidi kuimarika iwapo wanachama wa chama hicho watatekeleza na kusimamia vyema katiba yao kwa kulipa ada ya uanachama kwa wakati.

Alisema nguvu hizo ni vyema zikaunganishwa sambamba na vikao vya chama hicho vitakavyoitishwa kwa mujibu wa kanuni kulingana na ngazi zinazo husika kwa wanachama hao.
Balozi Seif alisema hayo wakati wa ziara yake ya kuimarisha Chama ndani ya Mkoa wa Magharibi akiwa pia mlezi wa Mkoa huo wakati akizungumza na viongozi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mfenesini hapo Ofisi ya CCM Wilaya Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alieleza kwamba mwanachama ana haki ya kumuomba Katibu wake ngazi yoyote kuitisha Mkutano wa wanachama kujadili jambo atakaloliwasilisha kama litakuwa na umuhimu mkubwa kwa maslahi ya Chama chenyewe.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alifahamisha kwamba kwa  utaratibu huo chama hicho kitaendelea kuwa madhubuti jamb o ambalo litakuwa tishio kwa upande wa upinzani kisiasa.


“ Chama chetu kwa utaratibu huu kitaendelea kuwa madhubuti na tishio kwa kambi yoyote ile ya upinzani hapa Nchini “. Alieleza Balozi Seif.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Mohd Yussuf alimuhakikishia mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kwamba Majimbo yote mawili yaliyoazimwa upande wa upinzani katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 yatarudi CCM Mwaka 2015.

Mapema asubuhi Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif akilitembelea Shina nambari Nane la CCM Tawi la Sharibu Msa aliwapongeza wanachama na Viongozi wa Shina hilo kwa umadhubuti wao wa kutekeleza katiba ya ccm kwa vitendo.

Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kinaendelea kuthamini ngazi ya mashina ambayo ndio msingi na muhimili pekee wa chama hicho.

Aliwaeleza wana CCM hao wa Shina nambari nane Sharifu Msa kwamba Uongozi wa Juu wa CCM Zanzibar chini ya Makamu Mwenyekiti wake Dr. Ali Mohamed Shein unakusudia kuandaa utaratibu wa kukutana na wanachama wa mashina katika mpango wake wa kuimarisha Chama chao.

Balozi Seif aliutaka Uongozi wa Mashina kuhakikisha kwamba  kila mwanachama ana kadi ya Chama, kadi ya Mzanzibari Mkaazi na ile ya kupigia kura ili kuirahisishia CCM kuendelea kushinda katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.

Akitoa Taarifa ya utekelezaji wa kazi za Chama ndani ya shina hilo Kiongozi wa Shina hilo nambari nane Sharifu Msa Bibi Khadija Abubakari alisema shina hilo lenye wanachama 24 ni miongoni mwa shina linaloongoza katika utekelezaji wa sera na ilani ya chama cha Mapinduzi ndani ya Tawi hilo.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alianza ziara yake kwa kukutana na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharibi Meli sita Mwera ambapo katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Aziza Ramadhan Mapuri alisema upo ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa chama na ule wa Serikali Mkoani huo katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.