Mwashamba
Juma na Mwanrafia Kombo MCC
BARAZA la Wawakilishi jana lililazimika
kuahirisha kikao cha asubuhi kutokana na akidi ya wajumbe wa baraza hilo
kutotimia.
Mara baada ya Spika wa Baraza hilo, Pandu
Ameir Kificho, kuingia ukumbini na kukalia kiti chake akijiandaa kusoma dua ya
ufunguzi, alisimama na kusema asingeweza kuendelea na kikao kutokana na akidi
kutotimia na kusema anasitisha ili wajumbe wapate nafasi ya kutafutwa.
Wakati huo wajumbe waliokuwemo ukumbini
ni 17 tu kati ya wajumbe wote 82 wanaounda baraza hilo.
Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za baraza
toleo la mwaka 2012, Spika anaweza kusitisha shughuli za baraza kwa dakika tano
iwapo akidi haitatimia baada ya mjumbe yeyote kusimama na kumwambia Spika
kwamba akidi haitatimia.
Na baada ya wajumbe kurudi ukumbini na
kama bado akidi haitatimia, Spika au Mwenyekiti ana mamlaka ya kusitisha
shughuli za baraza kwa dakika 30.
Hata hivyo, katika mkutano wa jana, Spika
aliahirisha kwa dakika 30, lakini hata muda huo ulipofika wajumbe waliokuwepo
ukumbini walikuwa 25 tu akiwemo Spika
mwenyewe.
Kwa mujibu wa kifungu cha 82 kifungu
kidogo cha 2 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ili akidi itimie lazima kuwe
na wajumbe zaidi ya nusu ya wajumbe wote wa baraza ambapo ni wajumbe 42 kwa
kuwa baraza hilo lina wajumbe 82.
Aidha kifungu cha 72 kifungu kidogo cha 2
cha kanuni za kudumu za Baraza toleo la mwaka 2012, akidi itatimia iwapo
kutakuwa na wajumbe zaidi ya nusu ya wajumbe wote wa baraza.
Kikao cha jana kilisitishwa kwa sababu
kazi iliyotakikana kufanyika ilihusiana na maamuzi, yanayohitaji kutimia akidi
ya wajumbe.
Kikao cha jana asubuhi kilikuwa kipitishe vifungu
vya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati ambayo ililazimika kupitishwa
jioni na jioni walikuwa wapitishe bajeti ya Wizara ya Fedha.
Aidha kwa mujibu wa kanuni za baraza
kifungu cha 74 (2), mjumbe anaweza kupewa adhabu ya kukatwa posho la siku iwapo
hakuhudhuria kikao cha siku cha baraza bila ya ruhusa ya Spika au Mwenyekiti na
atakuwa amejifukuza barazani kama hatahudhuria mikutano mitatu bila sababu zinazotambuliwa
na Spika au Mwenyekiti.
Na iwapo alilipwa posho kabla, atakatwa
posho hilo kwenye stahiki zake.
No comments:
Post a Comment