Habari za Punde

Balozi Seif akabidhi vifaa vya ujenzi jimboni

  Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi   vifaa vya ujenzi  kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Tawi  la Chama cha Mapinduzi Kwa Gube Mfenesini.

Kulia ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa CCM wa Tawi la CCM la Kwa Gube Ndugu Salum Ali Mzee.
 Balozi Seif akizungumza na Wana CCM wa Tawi la Kwa Gube mara baada ya kukabidhi vifaa kuendeleza ujenzi wa Tawi hilo.

Kushoto yake ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Mwenyekiti wa Tawi la CCM Kwa Gube Nd. Sal;im Ali Mzee na kulia ya Balozi Seif ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa  ambaye pia Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “ B” Nd. Haji Makungu Mgongo.
 Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif akimkabidhi vifaa vya ujenzi Katibu wa Maskani ya CCM ya Mtakuja iliyopo Kazole Bibi Zena Issa  kwa ajili ya uendelezaji ujenzi wa Maskani hiyo.
 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi akiwashauri wana CCM, wa Matawi ya Jimbo hilo kuanzisha madarasa ya maandalizi ili kuwaondoshea usumbufu wa elimu watoto wao.

Kushoto ya Mama Asha ni Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi vifaa vya Ujenzi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Matetema Kazole  Mwalimu Ali Salim Ali ili kusaidia kuendeleza ujenzi wa jengo la pili la Skuli hiyo.

Picha na – OMPR – ZNZ.
 
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba juhudi za Wananchi wa Vijiji vya Matetema na Kwa Gube Mfenesini  ndani ya Jimbo la Kitope za kujenga Skuli sambamba na ongezeko na Madarasa linafaa kuungwa mkono na jamii.
 
Alisema kitendo cha wananchi hao kwa kiasi kikubwa kitaleta ukombozi kwa watoto wao hasa wale wa umri mdogo wa kufuata elimu katika Vijiji vya mbali masafa ambayo wakati mwengine yanawasababishia hatari ya maisha yao wakati wa kuvuka bara bara.
 
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo wakati akikabidhi vifaa vya ujenzi  kwa Uongozi wa Skuli ya Maandalizi ya Kwa Gube Mfenesini waliyoanza kwa hatua ya msingi wa jengo la Maandalizi pamoja na ule wa Skuli ya  Matetema unaoendelea na ujenzi wa jengo la Pili.
 
Vifaa vilivyotolewa kutokana na fedha za mfuko wa Jimbo ni Matofali elfu 2,600 kwa skuli ya Maandalizi Kwa Gube ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini  “ B “ imeonyesha nia ya kusaidia saruji, wakati Skuli ya Matetema ikakabidhiwa matofali 1,500, nondo,saruji fedha za fundi vitu vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 5,425,000/-.



Balozi  Seif alisema kwamba juhudi za uongozi wa jimbo hilo zitaendelea kufanywa ili kuona matatizo na changamoto zinazowakabili  wananchi wa Vijiji vilivyomo ndani ya Jimbo la Kitope  kama huduma za maji safi na salama, bara bara na umeme zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
 
Akizungumzia Kura ya Maoni baada ya kukabidhi vifaa vya ujenzi kwa baadhi ya Matawi na Maskani za CCM zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema kero na migogoro ya Muungano itamalizika ndani ya katiba iliyopendekezwa kama itapigiwa kura ya ndio.
 
Aliwatahadharisha wananchi kuwa macho na baadhi ya watu wanaotaka kuona maisha ya wananchi walio wengi hapa nchini yanakuwa katika mshaka, nakama na matatizo ya muda mrefu.
 
Alisema hakuna Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika historia ya Taifa hili yenye faida kwa umma kama hii iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba itakayowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kuipigia kura ya maoni.
 
Balozi Seif alifahamisha kwamba Katiba iliyopendekezwa na Bunge hilo imetowa nafasi kubwa kwa Zanzibar hasa katika mambo mengi yaliyokuwa yakileta kero la kulalamikiwa na Zanzibar katika kipindi kirefu kilichopita.
 
Alieleza kuwa Halmashauri  za CCM za Mikoa na Wilaya  pamoja na wabunge wa Bunge Maalum  wamejipanga vyema  kutoa taaluma kwa wananchi waielewe Katiba iliyopendekezwa ili iwe rahisi kuifahamu vizuri wakati wa kuipigia kura.
“ Chama cha Mapinduzi kitatoa uelewa kwa Viongozi wa Halmashauri za Mikoa na Wilaya ili nao baadaye wapate fursa za kuwaelimisha wananchi umuhimu wa Katiba iliyopendekezwa “. Alieleza Balozi Seif.
 
Mjumbe huyo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema amani na utulivu Nchini Tanzania itaendelea kudumu iwapo chama cha Mapinduzi  { CCM } kitaendelea kuongoza Taifa hili.
 
“ Ukosefu wa ushindi kwa chama tawala cha Mapinduzi  ni hatari kwa maisha na maendeleo ya wananchi walio wengi hapa Nchini “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Mapema Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi  aliwataka Viongozi wa CCM wa Matawi ya Jimbo hilo kuanzisha madarasa ya maandalizi ili kwenda sambamba na Sera ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ya kumpa fursa  kila mtoto wa Visiwa hivi  aanze elimu ya Maandalizi akijiandaa kwa elimu na Msingi.
 
Mama Asha alisema yeye akiwa kama mzazi na mwenye uchungu wa elimu amekubali kujitolea posho kwa Mwalimu atayekubali kujitolea kusimamia elimu ya watoto hao wa maandalizi.
 
Katika ziara hiyo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope alikabidhi vifaa vya ujenzi kwa Tawi la CCM Kwa Gube, Maskani ya CCM Kazole,Maskani ya Mtakuja Kazole, Tawi la CCM Kazole,Maskani ya Ndio Sie Sie ya Matetema pamoja na Timu ya Mpira wa Miguu ya Matetema iliyopatiwa fedha taslim kwa ununuzi wa Posi za Magol i pamoja na Nyavu.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.